MASOMO YA MISA, JULAI 10,
2021
JUMAMOSI, JUMA LA 14 LA
MWAKA
SOMO 1
Mwa. 48:29-33; 50:15-25
Yakobo aliwaamuru wanawe:
Mimi ninakwenda kukusanywa pamoja na watu wangu; mnizike pamoja na baba zangu,
katika pango iliyomo shambani mwa Efraoni, Mhiti; katika ile pango iliyomo
shambani mwa Makpela, iliyo mbele ya Mamre katika nchi ya Kanaani, aliyoinunua
Ibrahimu pamoja na shamba kwa Efraoni Mhiti, pawe milki yake pa kuzikia. Humo
walimzika Ibrahimu, na Sara mkewe; humo wakamzika Isaka, na Rebeka mkewe; nami
humo nikamzika Lea; shamba na pango iliyomo lililonunuliwa kwa bani Hethi.
Basi Yakobo alipokwisha
kuwaagiza wanawe, akakunja miguu yake kitandani, akafa, akakusanywa pamoja na
watu wake.
Ndugu zake Yusufu
walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye
atatulipa maovu yetu tuliyomtenda. Wakapeleka watu kwa Yusufu, kunena, baba
yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema, Mwambieni Yusufu hivi, Nakuomba
uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa
twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia
waliposema naye.
Nduguze wakaenda tena,
wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumwa wako. Yusufu akawaambia,
Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu? Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali
Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoka taifa kubwa, kama ilivyo leo.
Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha, na watoto wenu. Akawafariji, na kusema
nao vema.
Akakaa yusufu katika
Misri, yeye na nyumba ya babaye. Akaishi Yusufu miaka mia na kumi. Yusufu
akaona wana wa Efraimu hata kizazi cha tatu; na wana wa Makiri, mwana wa
Manase, alizaliwa magotini mwa Yusufu.
Yusufu akawaambia
nduguze, Mimi ninakufa, lakini Mungu atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha
kutoka nchi hii, mpaka nchi aliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, akaisema, Bila
shaka Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu.
Neno la Bwana… Tumshukuru
Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 105: 1-4, 6-7 (K)
69:32
(K) Enyi mmtafutao Mungu,
mioyo yenu ihuishwe.
Aleluya.
Mshukuruni Bwana,
liitieni jina lake,
Wajulisheni watu matendo
yake,
Mwimbieni, mwimbieni kwa
zaburi,
Zitafakarini ajabu zake
zote. (K)
Jisifuni kwa jina lake
takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao
Bwana.
Mtakeni Bwana na nguvu
zake,
Utafuteni uso wake siku
zote. (K)
Enyi wazao wa Ibrahimu,
mtumishi wake,
Enyi wana wa Yakobo
wateule wake.
Yeye Bwana, ndiye Mungu
wetu,
Duniani mwote mna hukumu
zake. (K)
SHANGILIO
1Pet. 1:25
Aleluya, aleluya,
Neno la Bwana hudumu hata
milele, na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya.
INJILI
Mt. 10:24 – 33
Yesu aliwafundisha mitume
wake: Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumwa hampiti bwana wake. Yamtosha
mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa
wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli; je! Si zaidi wale walio wa nyumbani mwake?
Basi, msiwaogope, kwa
maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa,
ambalo halitajulikana. Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na
msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba. Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze
kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia
katika jehanum. Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja
haanguki chini asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu
zimehesabiwa zote. Msiogope basi; bora nyinyi kuliko mashomoro wengi.
Basi, kila mtu
atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbel za Baba yangu aliye mbinguni.
Basil mtu yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba
yangu aliye mbinguni.
Neno la Bwana… Sifa kwako
Ee Kristo.
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see
www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment