“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Ijumaa, Julai 2, 2021,
Juma la 13 la Mwaka
Mwa 23:1-4,19,
24:1-8,62-67;
Zab 105: 1-5;
Mt 9: 9-13
MDHAMBI ANAKARIBISHWA KWA
HURUMA
Ndugu zangu wapendwa,
karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo katika tafakari ya
neno la Bwana, katika somo la kwanza, Abrahamu anapoteza mke wake kipenzi ndiye
Sara. Tukio hili linakuwa la uchungu sanaa kwake lakini yeye analipokea kwa
utulivu na imani na kumzika mke wake. utulivu wake unaonesha ukuu wa imani ya
Abrahamu. Matatizo haya hayamfanyi aanguke kiimani.
Ndugu zangu, Abrahamu
atupatie somo hasa sisi wakristo. Nyakati za matatizo zitatupata. Wakati
mwingine tunayumbishwa na vipindi vya matatizo na uchungu na kutufanya tupoteze
imani. Hivi havifai kutuyumbisha ndugu zangu. Tukumbuke kwamba nyakati za shida
zitatokea, nyakati za matatizo makubwa zitajitokeza katika maisha. Lakini
tunapaswa kumuiga Abrahamu. Tuoneshe utulivu mkubwa. Moyo uliojaa utulivu ni
dhihirisho la ukuu wa imani yetu.
Katika injili, Yesu
anamchagua mtoza ushuru, Matayo kuwa mfuasi wake. Mfuasi huyu kwa mwanzoni
hakupokeleka na wengi kwa sababu alikuwa mtumishi katika serikali ya
kirumi-serikali iliyochukiwa na Wayahudi kwa kiasi kikubwa kwani ilionekana
kuwa serikali dhalimu. Hivyo Matayo alionekana kuwa msaliti, aliyeitumikia
serikali ya kikoloni. Pia kwa kipindi hicho, watoza ushuru wengi walikuwa wala
rushwa kwani walitoza kingi zaidi ya kilichoagizwa. Jambo hili liliwachafua
sana na kuonekana kuwa watu wachafu. Lakini Bwana Yesu anakuwa tayari kumchagua
huyu kuwa mfuasi wake.
Hakika Matayo alipewa
heshima na upendeleo wa pekee na alipaswa kuupokea upendeleo huu kwa heshima
kubwa. Na hakika alipokea upendeleo huu vyema. Sisi tutambue kwamba upo wakati
Bwana Yesu anatuletea nafasi ya upendeleo, hasa wakati tunapokuwa katika dhambi
zetu. Yeye atajitokeza na kutoa nafasi ya upendeleo. Hata kama mtu ni mbaya
kiasi gani, tutambue kwamba upo wakati Bwana Yesu atatuletea nafasi ya
upendeleo.
Yafaa tujifunze kuzipokea
nafasi hizi vyema kama alivyofanya Matayo: Matayo aliacha kazi yake na
kumfuata, alipata upendeleo na kuacha matendo yake maovu. Nasi tufanye hivyo
hivyo. Nafasi ya upendeleo tuipatapo, tukubali kuacha matendo yetu ya giza na
kumfuata Bwana. Wengi tunaanguka kwa sababu hatujajifunza kupokea nafasi hizi
za upendeleo vyema. Tujitahidi.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment