MASOMO YA MISA,
IJUMAA, JULAI 2, 2021
JUMA LA 13 LA MWAKA
SOMO 1
Mwa. 23:1-4, 19; 24:1-8,
62-67
Umri wake Sara ulikuwa
miaka mia na ishirini na saba, ndio umri wake Sara. Sara akafa katika
Kiriath-arba, ndio Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Ibrahimu akaja kumlilia
Sara na kumwombolezea. Akaondoka Ibrahimu kutoka mbele ya maiti wake, akasema
na bani Hethi, akinena, Mimi ni mgeni, ninatembea kwenu; nipeni mahali pa
kuzikia kwenu, pawe pangu, nimzike maiti wangu atoke mbele yangu.
Basi baada ya hayo Ibrahimu
akamzika Sara mkewe katika pango ya shamba la Makpela kuelekea Mamre, ndiyo
Hebroni, katika nchi ya Kanaani.
Ibrahimu alikuwa mzee
mwenye miaka mingi, na Bwana alikuwa amembariki Ibrahimu katika vitu vyote.
Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake
vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu, nami nitakuapisha kwa
Bwana, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke
katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao; bali enenda hata nchi yangu, na
kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke. Yule mtumishi akamwambia, Labda
yule mwanamke hatakubali kufuatana nami mpaka nchi hii, Ibrahimu akamwambia,
Ujihadhari, usimrudishe mwanangu huko. Bwana, Mungu wa mbingu, aliyenitoa
katika nyumba ya babaangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia
akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako,
anwe utamtwalia mwanangu mke tokea huko; na yule mwanamke asipokubali kufuatana
nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki; lakini usimrudishe mwanangu huko.
Basi isaka alikuwa
amekuja kwa njia ya Beer-lahai-roi, maana laikaa katika nchi ya kusini. Isaka
akatoka ili kutafakari kondeni wakati wa jioni; akainua macho yake, akaona,
kuna ngamia wanakuja. Rebeka akainua macho, anaye alipomwona Isaka, alishuka
juu ya ngamia. Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye kondeni kutulaki?
Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika.
Yule mtumishi akamwambia Isaka mambo yote aliyoyatenda. Isaka akamwingiza
Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda;
Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamaake.
Neno la Bwana...
Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 106:1-5 (K) 1
(K) Mshukuruni Bwana kwa
kuwa ni mwema.
Aleluya.
Mshukuruni Bwana kwa kuwa
ni mwema,
kwa maana fadhili zake ni
za milele.
Nani awezaye kuyanena
matendo makuu ya Bwana,
kuzihubiri sifa zake
zote. (K)
Heri washikao hukumu,
Na kutenda haki sikuzote.
Ee Bwana, unikumbuke
mimi,
Kwa kibali uliyo nayo kwa
watu wako. (K)
Unijilie kwa wokovu wako,
Ili niuone wema wa
wateule wako.
Nipate kuifurahia furaha
ya taifa lako,
Na kujisifu pamoja na
watu wako. (K)
SHANGILIO
Zab. 130:5
Aleluya, aleluya,
Roho yangu inamngoja
Bwana,
na Neno lake nimelitumainia.
Aleluya.
INJILI
Mt. 9:9 – 13
Yesu alipokuwa akipita
kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate.
Akaondoka, akamfuata.
Ikawa alipoketi nyumbani
ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi
pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi
wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Naye
aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi.
Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si
sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.
Neno la Bwana........Sifa
kwako Ee Kristo
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see
www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment