Tafakari ya kila siku
Jumatano, Julai 23, 2025.
JUMA LA 16 LA MWAKA
Zab 78:18-19, 23-28;
Mt 13:1-9.
MBEGU NENO LA MUNGU!
Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo katika tafakari ya Neno la Bwana, wana wa Israeli wanapatwa na njaa jangwani na kuanza kutamani utumwa. Wana wa Israeli walipotoka Misri, walibeba vyakula mbalimbali lakini kwa wakati huu, vimeisha. Wanalalamika na kuanza kutamani chakula cha Wamisri.
Mungu atawanyeshea mkate
safi, mkate toka Mbinguni, Mana ili waile. Lakini muda sio mrefu, watakinai
chakula hiki na kuanza kutamani kile cha utumwani Misri na kusema ni kizuri
zaidi. Na Mwenyezi Mungu atakasirika na kuwaadhibu na mwishowe wale wote
watakaokataa kuila manna, watashindwa kufika katika nchi ya ahadi.
Ndugu zangu, sisi
changamoto kubwa inayotukabili kila siku ni kukinai sakramenti. Mara ya kwanza,
tunapokea sakramenti zetu kwa mwitikio mzuri, lakini baada ya muda, tunaanza
kukikanai na mwishowe nafasi ya skaramenti zetu inapotea. Hili ni suala
tunalopaswa kupambana nalo kwani wakristo wengi wameacha kupokea sakramenti,
hasa ekaristi kwa sababu wanadai hawaoni chochote cha ziada. Wamekinai
sakramenti hii. Lakini wanapaswa kuelewa kwamba sakramenti ni mafumbo
matakatifu yanayopaswa kupokelewa kiimani. Bila imani, huwezi kuiona nguvu ya
sakramenti zetu.
Hivyo tujitahidi
kupambana na ugonjwa wa kukinai sakramenti na hakika tutaweza kupata msaada wa
sakramenti zetu.
Katika somo la injili,
Yesu anatupatia mfano wa mpanzi kuelezea namna jinsi tulivyoruhusu mioyo yetu
kujifunua kuelewa ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Hakika wapo ambao tangu mwanzo hawakulipatia
nafasi neno la Mungu na mwishowe mbegu ilishindwa kuota au kuota na kukauka.
Hii ni changamoto inayowapata wakristo wengi sasa. Hakika neno la Mungu
halipatiwi nafasi na wengi wetu mbegu yetu inashindwa kuota au inaota na
kunyauka mara moja. Sisi tuangalie ni kipi kinachotufanya tushindwe kumpatia
Mwenyezi Mungu nafasi.
Urafiki mbaya, tamaa ya
fedha, uasherati, unafiki, kusengenya au kukosa unyoofu vyote hivi vyaweza kuwa
miongoni mwa vitu vinavyozuia mbegu ya imani kukua ndani mwetu. Lazima tuwe
tayari kupambana na mambo haya.
------------------------
Copyright ©2013-2025
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
🙏🏽
ReplyDelete