MASOMO YA MISA,
JUMATATU, JULAI 19, 2021
JUMA LA 16 LA MWAKA
SOMO 1
Kut. 14: 5-18
Mfalme wa Misri aliambiwa
ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi
wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili
tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena? Akaandalia
gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye; tena akatwaa magari mia sita
yaliyochaguliwa, na magari vote ya Misri, na maakida juu ya magari hayo vote.
Na Bwana akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata
wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri. Wamisri
wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye
kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu na
bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni. Hata Farao alipokaribia,
wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao;
wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia Bwana.
Wakamwambia Musa, Je! kwa
sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona
umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri? Neno hili silo tulilokuambia
huko Misri, tukisema, Tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia
Wamisri kuliko kufa jangwani. Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu,
mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo
hamtawaona tena milele. Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.
Bwana akamwambia Musa,
Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele. Nawe inua fimbo
yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli
watapita kati ya bahari katika nchi kavu. Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya
Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa
Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake. Na
Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapokwisha kujipatia utukufu kwa
Farao, na magari yake, na farasi zake.
Neno la
Mungu...Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATIKATI
Kut. 15 :1-6 (K) 1
(K) Nitamwimbia Bwana,
kwa maana ametukuka sana.
Nitamwimbia Bwana, kwa
maana ametukuka sana;
Farasi na mpanda farasi
amewatupa baharini.
Bwana ni nguvu zangu, na
wimbo wangu;
Naye amekuwa wokovu
wangu.
Yeye ni Mungu wangu, nami
nitamsifu;
Ni Mungu wa baba yangu,
nami nitamtukuza. (K)
Bwana ni mtu wa vita,
Bwana ndilo jina lake.
Magari ya Farao na jeshi
lake amewatupa baharini,
Maakida yake wateule
wamezama katika bahari ya Shamu. (K)
Vilindi vimewafunikiza,
Walizama vilindini kama
jiwe.
Bwana, mkono wako wa
kuume
umepata fahari ya uwezo,
Bwana, mkono wako wa kuume
wawasetaseta adui. (K)
SHANGILIO
Yn 15:15
Aleluya, aleluya,
Bwana anasema: Siwaiti
tena watumwa,
lakini ninyi nimewaita
rafiki,
kwa kuwa yote
niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu. Aleluya.
INJILI
Mt. 12:38-42
Baadhi ya waandishi wa
Mafarisayo walimjibu Yesu wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako.
Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala
hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona. Kwani kama vile Yona alivyokuwa
siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu
atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi. Watu wa Ninawi
watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa
wamekosa; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu
kuliko Yona. Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi
hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za
mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.
Neno la Bwana...Sifa
kwako, ee Kristo
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment