MASOMO YA MISA,
JUMATANO, JULAI 28, 2021
JUMA LA 17 LA MWAKA
SOMO 1
Kut. 34 : 29-35
Hata ikawa, Musa
aliposhuka katika mlima Sinai, na ztie mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi
mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake
iling’aa kwa sababu amesema na Bwana. Basi Haruni na wana wote wa Israeli
walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake iling’aa; nao wakaogopa kumkaribia.
Musa akawaita; Haruni na wakuu wote wa kusanyiko wakarudi kwake; Musa akasema
nao.
Baadaye wana wa Israeli
wote wakakaribia; akawausia maneno yote ambayo Bwana amemwambia katika mlima
Sinai. Na Musa alipokuwa amekwisha kusema nao, akatia utaji juu ya uso wake.
Lakini desturi ya Musa ilikuwa alipoingia mbele za Bwana kusema naye, kuuvua
huo utaji mpaka atoke; akatoka akawaambia wana wa Israeli maneno yote
aliyoambiwa. Wana wa Israeli wakauona uso wa Musa ya kuwa ngozi ya uso wake
Musa iling’aa; naye Musa akautia utaji juu ya uso wake tena, hata alipoingia
kusema naye.
Neno la
Mungu...Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 99: 5-7, 9 (K)9
(K) Bwana, Mungu wetu,
ndiye mtakatifu.
Mtukuzeni Bwana, Mungu
wetu,
sujuduni penye kiti cha
miguu yake, ndiye mtakatifu. (K)
Musa na Haruni miongoni
mwa makuhani wake,
na Samweli miongoni mwao
waliitiao jina lake,
walipomwita Bwana
aliwaitikia. (K)
Katika nguzo ya wingu
alikuwa akisema nao.
Walishika shuhuda zake na
amri aliyowapa. (K)
Mtukuzeni Bwana, Mungu
wetu,
sujuduni mkiukabili mlima
wake mtakatifu,
maana Bwana, Mungu wetu,
ndiye mtakatifu. (K)
SHANGILIO
Yak 1:18
Aleluya, aleluya, Kwa
kupenda kwake mwenyewe, Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko
la viumbe vyake. Aleluya.
INJILI
Mt. 13 :44-46
Yesu aliwaambia makutano
mifano, Ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba;
ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo
vyote, akalinunua shamba lile. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya
biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa,
alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua.
Neno la Bwana...Sifa
kwako, ee Kristo
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment