“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumatano Julai 28, 2021
Juma la 17 la Mwaka
Kut 34:29-35
Zab 99:5-7, 9;
Mt 13:44-46
KUTAFUTA LULU YA THAMANI
KUBWA
Karibuni sana wapendwa
kwa adhimisho la misa takatifu katika asubuhi ya leo. Leo katika tafakari ya
neno la Bwana, katika somo la kwanza, Musa anatokea mbele ya watu, baada ya
kukaa mlimani kwa siku arobaini usiku na mchana. Anapotokea mbele ya wana wa
Israeli, uso wake unaonekana kungaa, na wana wa Israeli wanaoona hili,
wanaogopa. Lakini Musa hakujua kwamba kwa kitendo cha uso wake kungaa,
kiliwafanya wana wa Israeli waogope, yeye aliona kwamba ni jambo la kawaida, na
hakujiona kungaa. Na alikuwa akienda mbele ya wana wa Israeli kama kawaida bila
kujitambua kwamba kungaa kwa uso wake kuliwatisha.
Kungaa huku kulimaanisha
kwamba Musa amepokea sehemu ya utukufu wa Bwana, kwa sababu alikaa na Bwana
usiku na mchana juu ya mlima Sinai kwa siku arobaini mchana na usiku. Hivyo ule
utukufu wa Bwana ulikuwa juu yake. Kungaa huku kulimfanya apate madaraka mbele
ya wana wa Israeli, waepuke kufikiria kana kwamba hakutumwa. Hapa ni Mungu
alimdhihirisha kwamba yeye ni mtume wake mpendwa hivyo asikilizwe. Musa
alipaswa kutunza kungara huku kwake sura akijua kwamba yeye ni kiumbe
kitakatifu cha Mungu na hivyo yafaa atimize kazi ya Bwana.
Nasi tumepokea sehemu ya
utukufu wa Bwana, Bwana ametushirikisha utukufu wake, kungaa kwake kwa ubatizo
wetu na baadaye kipaimara. Tuheshimu utukufu huu. Tusijichanganye au kujitoa
kwa shetani. Maisha yetu yawe kwa ajili ya Bwana ili Bwana atusaidie. Ni kufuru
kubwa ikiwa tutaruhusu utukufu wetu uchangamanike na maisha ya kishetani. Musa alijifunika
uso wake mbele ya watu ili watu wasidharau utukufu huu, kama sehemu ya heshima.
Nasi tunapaswa kufanya hivyo hivyo; tusichukulie utukufu wetu, ubatizo wetu,
maisha yetu ya wakfu, kama kitu cha kawaida sana; tunapaswa kuupatia heshima
zake zote. Tukiona kila kitu katika ukawaida, hakika tutashindwa kumpatia Mungu
wetu sifa na heshima yake.
Katika injili, Yesu
anafananisha ufalme wa mbinguni na mfanyabiashara atafutaye lulu zuri na
akishajua sehemu iliyojificha, huuza yote ili kuipata lulu hiyo. Yesu ndiye
mwenye kufanya sadaka ya namna hii. Yeye ndiye mwenye kukubali kutoa yote apate
kuikomboa roho ya mwanadamu na kutupatia wokovu. Alikuwa tayari kutoa maisha
yake kama sadaka. Nasi tuwe watu wa kukubali kuacha yote ili kujitoa kwa Yesu.
Tumsifu Yesu Kristo.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment