MASOMO YA MISA,
JUMANNE, JULAI 6, 2021
JUMA LA 14 LA MWAKA
Kumbukumbu ya Mtakatifu
Benedikto, Abati
SOMO 1
Mwa. 32:23-33
Yakobo aliondoka usiku
ule akawatwaa wakeze wawili, na vijakazi wake wawili, na wanawe kumi na mmoja,
akavuka kivuko cha Yaboki. Akawatwaa, akawavusha mto, akavusha na vyote
alivyokuwa navyo.
Yakobo akakaa peke yake;
na mtu mmoja akashindana naye mweleka hata alfajiri. Naye alipoona ya kuwa
hamshindi, alimgusu panapo uvungu wa paja lake; ukateguka uvungu wa paja la
Yakobo alipokuwa akishindana naye. Akasema, Niache, niende, maana
kunapambazuka. Akasema, Sikuachi, usiponibariki. Akamwuliza, Jina lako n’nani?
Akasema, Yakobo. Akamwambia, Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana
umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda. Yakobo akamwuliza, akasema,
Niambie, tafadhali, jina lako? Akasema, Kwa nini waniuliza jina langu?
Akambariki huko.
Yakobo akapaita mahali
pale, Penueli, maana alisema, Nimeonana na Mungu uso kwa uso, na nafsi vangu
imeokoka. Jua likamzukia akivuka Penueli, akachechemea kwa sababu ya paja la
mguu wake. Kwa hiyo wana wa Israeli hawali ule mshipa ulio katika uvungu wa
paja hata leo; maana alimgusa Yakobo panapo uvungu wa paja katika mshipa wa
kiuno.
Neno la Bwana… Tumshukuru
Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 17 :1-3, 6-8, 15 (K)
15
(K) Nikutazame uso wako
katika haki..
Ee Bwana, usikie haki,
ukisikilize kilio changu,
Utege sikio lako kwa
maombi yangu,
Yasiyotoka katika midomo
ya hila. (K)
Hukumu yangu na itoke
kwako,
Macho yako na yatazame
mambo ya adili.
Umenijaribu moyo wangu,
umenijilia usiku,
Umenihakikisha usione
neno;
Nimenuia kinywa changu
kisikose. (K)
Ee Mungu, nimekuita kwa
maana utaitika,
Utege sikio lako ulisikie
neno langu.
Dhihirisha fadhili zako
za ajabu,
Wewe uwaokoaye
wanaokukimbilia;
Kwa mkono wako wa kuume
Uwaokoe nao
wanaowaondokea. (K )
Unifiche chini ya uvuli
wa mbawa zako;
mimi nikutazame uso wako
katika haki,
Niamkapo nishibishwe kwa
sura yako. (K)
SHANGILIO
Yn. 10 : 27
Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia
sauti yangu,
nami nawajua, nao
wanifuata.
Aleluya.
INJILI
Mt. 9: 32-39
Walimletea Yesu mtu bubu
mwenye pepo. Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wa kastaajabu,
wakasema, Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wo wote. Lakini Mafarisayo
wakisema, Kwa nguvu za mkuu wa pepo atoa pepo.
Naye Yesu alikuwa
akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na
kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila
aina.
Na alipowaona makutano,
aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kondoo wasio na
mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda
kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika
mavuno yake.
Neno la Bwana........Sifa
kwako Ee Kristo
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see
www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment