"ASALI ITOKAYO
MWAMBANI"
Tafakari ya kila siku
Jumanne, Julai 6, 2021,
Juma la 14 la Mwaka
Kumbukumbu ya Mt.
Benedikto, Abati
Mwa 32:23-33;
Zab 16:1-3, 6-8;
Mt 9:32-37
KUSIMAMA IMARA KATIKATI
YAVIPINGAMIZI!
Ndugu zangu wapendwa,
karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika
somo la kwanza tunakutana na Yakobo akiendelea kuneemesha maisha yake na
kuyapatia baraka. Leo katika masomo yetu anaonekana kuwa mtu wa bidii aliyekuwa
na uchu wa kubarikiwa. Aliogopa sana laana maishani mwake. Kila aliyekutana
naye alijitahidi kuomba baraka.
Alipendezwa kuwa na sifa
nzuri na baraka maishani. Na leo Mwenyezi Mungu anabadili jina lake toka Yakobo
kwenda Israeli kumaanisha kwamba hakika amekuwa kiumbe kipya cha Bwana chenye
kubarikiwa naye na kupokea wingi wa neema zake. Nasi tuwe watu wa kuomba baraka
za Mwenyezi Mungu maishani. Tunaokaa nao tuishi nao vyema ili tupate baraka
toka kwao. Kama ni wagonjwa tunawatunza, tuwatunze kwa roho nzuri ili tuchote
toka kwao baraka. Kama ni wafungwa, wazee, yafaa tuwatunze vyema na kuchota
kwao baraka; tuwabembeleze tupate toka kwao baraka na sio laana. Maisha ya
wengi wetu imejaa mikosi na shida kwa sababu ya kushindwa kubembeleza baraka
toka kwa wenzetu. Tusikubali vinywa vyetu viwe sababu ya sisi kulaaniwa.
Katika somo la injili,
baadhi ya Wafarisayo wanamkejeli Yesu kwamba anatoa pepo kwa nguvu ya Mkuu wa
pepo. Wivu wa Wafarisayo uliwafanya washindwe kuelewa juu ya ukuu wa nguvu ya
Mungu. Mwishowe wakaona kwamba shetani ni mwenye nguvu kuliko Mungu. Ndivyo
wivu ulivyombaya ndugu zangu. Wivu hutufanya tuone kwamba shetani ni Mwenye
nguvu sana na kila mahali anafanya kazi kuu. Lakini tunashindwa kuona nguvu ya
Mwenyezi Mungu maishani mwetu na maishani mwa maisha ya wengine. Hii ndio
hasara ya wivu. Mwenzetu akifanikiwa, wivu utatutuma kusema kwamba ni Freemason
na kushindwa kuona kwamba Mungu aweza kufanya kazi ndani ya maisha yake pia. Hivyo
tujue kwamba wivu wetu ndio utakaompatia shetani mamlaka.
Dunia bado inahitaji watu
wanaopaswa kuwaelimisha wengine hasara za mambo haya. Tuache kukumbatia vitabia
hivi vya wivu. Hakika ni vitabia hatari sana kwa maisha yetu. Tumwombe Bwana
atume wafanyakazi wengi katika shamba lake ili watusaidie katika kutuelewesha
hasara za mambo haya.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment