Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JULAI 8, 2021

 

MASOMO YA MISA, JULAI 8, 2021

ALHAMISI, JUMA LA 14 LA MWAKA

SOMO 1

Mwa. 44:18-21, 23-29; 45:1-5

Yuda alimkaribia Yusufu akasema, Tafadhali, bwana wangu, mtumwa wako na aseme neno moja masikioni mwa bwana wangu, wala hasira yako isimwakie mtumwa wako, maana wewe u kama FArao. Wewe, bwana wangu, ulituuliza watumwa wako, ukisema, Je! Mnaye baba, au ndugu? Tukakuambia wewe, bwana wangu, Tunaye baba, naye ni mzee, na mwana wa uzee wake ni mdogo, na nduguye amekufa; amebaki yeye peke yake wa katika tumbo la mamaye, na baba yake anampenda. Ukatuambia watumwa wako, Mleteni kwangu, ili macho yangu yamwangalie. Asiposhuka ndugu yenu mdogo pamoja nanyi, hamtaniona uso wangu tena. Ikawa tulipokwenda kwa mtumwa wako, baba yangu, tukamwarifu maneno yako, bwana wangu. Kisha baba yetu akanena, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo. Tukasema, Hatuwezi kwenda; ndugu yetu mdogo akiwapo pamoja nasi, tutashuka; maana hatutaweza kuuona uso wa mtu huyo, ndugu yetu mdogo asipokuwa pamoja nasi. Mtumwa wako, baba yangu, akatuambia, Mnajua ya kuwa mke wangu alinizaliwa wana wawili; mmoja alitoka kwangu, nikasema, Bilas haka ameraruliwa, wala sikumwona tangu hapo. Na mkiniondolea huyu naye, na madhara yakimpata, mtashusha mvi zangu na msiba kaburini.

Hapo Yusufu hakuweza kujizuia mbele yao wote waliosimama karibu naye. Akapiga kelele, na kusema, Mwondoeni kila mtu mbele yangu. Wala hakusimama mtu pamoja naye, Yusufu alipojitambulisha kwa nduguze. Akapaza sauti yake akalia, nao WAmisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia.

Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi ndimi Yusufu; baba yangu angali hai bado? Wala ndugu zake hawakuweza kumjibu, maana waliingiwa na hofu mbele yake. Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema, mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. Basi sasa, msihuzunike, wal amsiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 105:16-21 (K) 5

(K) Zikumbukeni ajabu Bwana alizozifanya.

Au: Aleluya.

Bwana aliita njaa iijilie nchi,

Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.

Alimpeleka mtu mbele yao,

Yusufu aliuzwa utumwani. (K)

Walimwumiza miguu yake kwa pingu,

Akatiwa katika minyororo ya chuma.

Hata wakati wa kuwadia neno lake,

Ahadi ya Bwana ilimjaribu. (K)

Mfalme alituma watu akamfungua,

Mkuu wa watu akamwachia.

Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake,

Na mwenye amri juu ya mali zake zote. (K)

SHANGILIO

Ebr. 4:12

Aleluya, aleluya,

Neno la Mungu li hai tena li na nguvu, li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.

Aleluya.

INJILI

Mt. 10: 7 – 15

Yesu aliwaambia mitume wake: Katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takasene wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure. Msichukue dhahabu, wala fedha wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake.

Na mji wowote au kijiji chochote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; make kwake hata mtakapotoka. Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni. Na nyumba ile ikistahili, Amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, Amani yenu na iwarudie ninyi. Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung’uteni mavumbi ya miguuni mwenu. Amin, nawambia, Itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

 

Copyright © 2020, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment