"ASALI ITOKAYO
MWAMBANI"
Tafakari ya kila siku
Alhamisi, Julai 8, 2021,
Juma la 14 la Mwaka
Mwa 44:18-21, 23-29;
45:1-5;
Zab 104:16-21;
Mt 10:7-15
KUPEWA NGUVU NA INJILI
Karibuni sana ndugu zangu
wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu ya
neno la Bwana katika somo la kwanza Yusufu anaonesha moyo wa huruma na
masikitiko kwa wenzao. Nao ndugu zake ambao hapo awali walimuuza Misri nao
wanapatwa na aibu kubwa na mshtuko kwamba waliyetegemea kwamba wamemwangamiza,
kumbe kwa sasa ametokea mbele yao kama mkuu, mwenye mamlaka makubwa mbele yao
ambao kwa sasa hawawezi tena kuyashinda.
Wakati akiwa mdogo, kaka
zake walikuwa na umbo na umri mkubwa na hivyo walitumia nguvu zao kumfanyia
ukatili. Lakini sasa Yusufu amekwishakuwa mkubwa na ni mwenye mamlaka makubwa;
analo pia na jeshi kubwa ambalo kwa sasa hawawezi kumshinda. Hakika ndugu zake
walipata mshtuko mkubwa.
Huu ni mwaliko kwetu
kwamba tuwaheshimu wote. Hata wadogo tulio nao tuwatunze vyema. Tusiwadhulumu
kipindi hiki walipo wadogo na dhaifu. Muda sio mrefu nao watapata nguvu pia.
Tusitumie miili yetu mikubwa kuwanyanyasa au kuwatendea uovu wowote. Yusufu
anakataa kuonesha moyo wa kisasi kwa nduguze. Alitambua kwamba Mwenyezi Mungu
ameamua kufanya haya akiwa na lengo maalumu. Hivyo aliweka imani mbele kuliko
visasi. Hili lilimfanya azidi kubarikwa zaidi.
Nasi tutambue kwamba
tutabarikiwa kwa kuepuka visasi. Wale tuliowahi kunyanyaswa halafu baadaye
tukafanikiwa-tutambue kwamba tutapata mafanikio zaidi pale tutakapoweza kuondoa
visasi na kuweka imani mbele kuliko chuki. Tusikubali kuzima baraka zetu kwa
njia ya visasi.
Katika somo la injili,
Yesu anatoa maagizo kwa wanafunzi wake namna ya kuihubiri injili. Katika
kuihubiri injiili, anasisitiza kwamba waweke injili mstari wa mbele kuliko
yote. Wamtegemee Mungu, wasikubali kulimbikiza ya dunia. Kazi ya Bwana ni
rahisi kusahauliwa kirahisi au kufunikwa na mambo ya dunia. Hivyo yafaa mambo
ya Mungu yapewe kipaumbele. Hatari hii ndio tunayoiona hadi nyakati zetu. Kazi
ya Bwana haipewi kipaumbele. Mambo ya dunia yanaifunika injili. Hata sisi tupo
tayari kukosa kanisani, au kupunguza muda wa sala ili tupate kufanya biashara
au harambee fulani. Hatupaswi kufunika mambo ya Mungu kwa malimwengu.
Malimwengu ni hatari kwa uenezi wa injili ya Bwana.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment