Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JULAI 7, 2021

 

MASOMO YA MISA, JULAI 7, 2021

JUMATANO, JUMA LA 14 LA MWAKA

SOMO 1

Mwa. 41:55-57; 42:5-7, 17-24

Nchi yote ya Misri ilipoona njaa, watu walimlilia Farao awape chakula. Farao akawaambia Wamisri wote. Enendeni kwa Yusufu; atakavyowaambia, fanyeni. Njaa ikawa katika dunia yote pia. Yusufu akazifungua ghala zote, akawauzia WAmisri. Njaa ikawa nzito katika nchi ya Misri. Watu wa nchi zote wakaja Misri kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote.

Wana wa Israeli wakaja wanunue chakula miongoni mwao waliokuja, kwa kuwa kulikuwa na njaa katika nchi ya Kanaani. Naye Yusufu alikuwa ni liwali juu ya nchi, ndiye aliyewauzia watu wote wa nchi. Nao ndugu zake Yusufu wakaja, wakainama kifudifudi mbele yake. Yusufu akawaona nduguze, akawatambua, lakini alijifanya kama mgeni kwao. Akasema nao kwa maneno makali, akawaambia, Mmetoka wapi ninyi? Wakasema, Tumetooka nchi ya Kanaani, ili tununue chakula.

Akawatia wote gerezani siku tatu. Yusufu akawaambia siku ya tatu, Fanyeni hivi, mkaishi, maana mimi namcha Mungu. Kama ni wa kweli ninyi, ndugu yenu mmoja na afungwe gerezani, nanyi nendeni mkachukue nafaka kwa njaa ya nyumba zenu, mkamlete ndugu yenu mdogo kwangu; hivyo maneno yenu yatahakikishwa, wala hamtakufa. Ndivyo walivyofanya. Wakaambiana, Kweli sisi tuliomkosa ndugu yetu, kwa kuwa tuliona shida ya roho yake alipotusihi, wal ahatukusikia; kwa hiyo shida hii imetupata. Reubeni akajibu, akawaambia, Sikuwaambia, nikisema, msimkose kijana? Wala hamkusikia; kwa hiyo damu yake inatakwa tena. Wal ahawakujua ya kwmba yusufu anawasikia, kwa sababu alikuwapo mkalimali kati yao. Akajitenga nao akalia. Kisha akawarudia, na kusema nao, akamtwaa Simeoni miongoni mwao, akamfunga mbele ya macho yao.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 33:1-2, 10-11, 18-19 (K) 22

(K) Ee Bwana fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe.

Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki,

Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.

Mshukuruni Bwana kwa kinubi,

Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa. (K)

Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa,

Huyatangua makusudi ya watu.

Shauri la bwana lasimama milele,

Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi. (K)

Tazama jicho la Bwana li kwa wamchao,

Wazingojeao fadhili zake.

Yeye huwaponya nafsi zao na mauti

Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)

SHANGILIO

Kol. 3:16,17

Aleluya, aleluya,

Neno la Kristu likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkishukuru Mungu Baba kwa Yeye.

Aleluya.

INJILI

Mt. 10:1 – 7

Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya; Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye; Yakobo wa Zebedayo, na Yohane nduguye; Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo; Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, naye ndiye mwenye kumsaliti. Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema.

Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wowote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kodnoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Copyright © 2020, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment