"ASALI ITOKAYO
MWAMBANI"
Tafakari ya kila siku
Jumatano, Julai 7, 2021,
Juma la 14 la Mwaka
Mwa 41:55-57; 42:5-7,
17-24;
Zab 32:2-3, 10-11, 18-19;
Mt 10:1-7
IMANI YA MFUASI
Karibuni sana ndugu
wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo
katika somo la kwanza tunakutana na tukio jinsi chuki na matendo yetu maovu
yawezavyo kuwa sababu ya kuturudisha nyuma kimaendeleo.
Wana wa Yakobo walimuuza
ndugu yao nchini Misri. Ndugu huyu (Yusufu) alikuwa na vipaji vingi, alikuwa na
uwezo wa kupata maono mbalimbali na hakika baraka ya Mungu ilikuwa juu yake. Na
kama hawa ndugu zake wangalimpokea na kushirikiana naye, kwa hakika wangekuwa
mbali sana, wao wenyewe wangesaidika. Lakini cha ajabu hili liliwafanya wamchukie
na hata kuamua kumuuza. Wanapomuuza, Mungu anazidi kumbariki; anakwenda
kuvitumia vipaji vyake na baraka zake kwa watu wa taifa jingine.
Anaifanya Misri iendelee
na Israeli irudi nyuma. Mwisho wa siku wanapata njaa na kwenda kuomba nchini
Misri. Lakini ukisoma aliyesaidia kuiletea nchi ya Misri maendeleo na kuwa na
akiba kubwa ya chakula ni huyu Yusufu aliyeuzwa na ndugu zake. Haya ndiyo
yanayotokea hadi nyakati zetu. Wivu unatufanya tusiwe tayari kuwapokea wenzetu
wenye ujuzi, tunaona wivu wa vipaji vyao vya uongozi, shuleni na katika jamiii.
Mwisho wa siku tunadumaza maendeleo yetu wenyewe.
Baadhi ya wataalamu
wanaweza wakakataliwa na sisi, labda kwa sababu ya chuki na hata kuwafukuza
katika jamii yetu. Lakini mwisho wa siku wanakwenda kuleta maendeleo sehemu
nyingine na mwishowe tunakwenda kuwa ombaomba kwao. Baadhi ya wataalamu
walikataliwa katika nchi zao na kwenda kuleta maendeleo katika nchi nyingine.
Mwisho wa siku tunakwenda kuomba msaada toka kwa hizi nchi. Lakini wataalamu
wanaotumika ni wa kutoka katika nchi zetu hizi. Hivyo tujifunze sana kuondoa
tabia za wivu. Wivu umezikosesha jamii zetu maendeleo. Wivu unatufanya turudi
nyuma kimaendeleo. Tuondokane na tabia hizi.
Katika somo la injili,
Yesu anawaita wanafunzi wake na kuwapa amri juu ya pepo wabaya na juu ya
wagonjwa wote. Aliwaambia waanze na watu wa Israeli, wale waliokaribu kabisa
kabla ya kwenda kwa watu wa mataifa. Waanze na nyumbani kwao kwanza, waimarishe
nyumbani na ndio watoke nje. Nyumbani wakishindwa, basi ndio waende kwa watu wa
mataifa. Sisi pia tunaalikwa kuiga walichoagizwa mitume. Yafaa tuanze na
familia zetu, tuimarishe familia zetu kwanza kabla ya kwenda kwa wenzetu.
Viongozi yafaa waimarishe
familia zao kwanza kabla ya kwenda kwa wenzao. Hii ni kwa sababu wengi wetu tunashindwa
kusikilizwa pale tutoapo ujumbe kwa sababu hata kile tunachokihubiri hakifuatwi
na watu wa nyumbani kwetu na mbaya zaidi hakifuatwi hata na sisi wenyewe. Yafaa
tuanze kujihubiria sisi wenyewe kabla ya kwenda kwa wenzetu. Tumsifu Yesu
kristo.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment