MASOMO YA MISA, JULAI 29,
2021
ALHAMISI, JUMA LA 17 LA
MWAKA
SOMO 1
Kut. 40:16-21, 34-38
Musa alifanya hayo yote;
kama yote Bwana aliyoagiza ndivyo alivyofanya. Hata mwezi wa kwanza wa mwaka wa
pili, siku ya kwanza ya mwezi, ile maskani ilisimamishwa. Musa akaisimamisha
maskani, akayaweka matako yake, akazisimamisha nguzo zake. Akaitanda hema juu
ya maskani, akakitia kifuniko cha hema juu yake; kama Bwana alivyomwamuru Musa.
Akautwaa ule ushuhuda, akautia ndani ya sanduku, akaiweka miti ya kuchukulia
juu ya sanduku, akakiweka kiti cha rehema juu ya sanduku, kisha akalileta
sanduku akalitia ndani ya maskani, naye akalitundika pazia la sitara,
akalisitiri sanduku la ushuhuda; kama Bwana alivyomwamuru Musa.
Ndipo lile wingu
likaifunikiza hema ya kukutania, na huo utukufu wa Bwana ukaijaza maskani. Wala
Musa hakuweza kuliingia hema la kukutania, kwa sababu lile wingu lilikaa juu
yake, na huo utukufu wa Bwana ukaijaza maskani.
Hapo lile wingu
lilipoinuliwa kutoka juu ya maskani, wana wa Israeli wakaenda mbele katika
safari zao zote, bali kama lile wingu halikuinuliwa, wakati ule hawakusafiri
hata siku ile lilipoinuliwa tena. Kwa maana lile wingu la Bwana lilikuwa juu ya
maskani wakati wa mchana, na mlikuwa na moto ndani yake wakati wa usiku, mbele
ya macho ya nyumba ya Israeli katika safari zao zote.
Neno la Bwana...
Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 84:2-5, 7, 10 (K) 1
(K) Maskani zako
zapendeza kama nini, Ee Bwana wa majeshi.
Nafsi yangu imezionea
shauku nyua za Bwana,
Naam, na kuzikondea,
Moyo wangu na mwili wangu
Vinamlilia Mungu aliye
hai. (K)
Shomoro naye ameona
nyumba,
Na mbayuwayu amejipatia
kito,
Alipoweka makinda yake,
Kwenye madhabahu zako, Ee
Bwana wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu
wangu. (K)
Heri wakaao nyumbani
mwako,
Wanakuhimidi daima.
Heri ambaye nguvu zake
zatoka kwako,
Na njia ziendazo Sayuni
zimo moyoni mwake.
Huendelea toka nguvu hata
nguvu,
Huonekana Sayuni kila
mmoja mbele za Mungu. (K)
Hakika siku moja katika
nyua zako
Ni bora kuliko siku elfu.
Ningependa kuwa bawabu
Nyumbani mwa Mungu wangu.
(K)
SHANGILIO
1 Pet. 1:25
Aleluya, aleluya,
Neno la Bwana hudumu hata
milele, na neno hilo ni neno jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya.
INJILI
Mt. 13:47 – 53
Yesu aliwaambia wanafunzi
wake: Ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya
wa kila namna; hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio
wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho
wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa
katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu
hayo yote? Wakamwambia, Naam. Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi
mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika
hazina yake vitu vipya na vya kale.
Ikawa Yesu alipoimaliza
mifano hiyo, alitoka akaenda zake.
Neno la Bwana... Sifa
kwako Ee Kristo.
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment