“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Alhamisi Juali 29, 2021
Juma la 17 la Mwaka
Kut 40:16-21, 34-38
Zab 84: 2-5, 7, 10 (K)
Mt. 13:47-53
KUUTAFUTA UFALME
Ndugu Zangu wapendwa,
karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika
somo la kwanza, Musa anaamriwa kutengeneza sanduku la agano na kuliweka katika
hema ya kukutania. Sanduku la agano liliashiria uwepo wa Mungu katika safari ya
maisha ya wana wa Israeli. Hivyo walilitegemea katika maongozi yao ya safari ya
kuelekea nchi ya ahadi. Bila uwepo wa Mungu katika safari yao, wana wa Israeli
wangalishindwa kuelekea katika njia salama.
Kama wana wa Israeli
walivyofumbuliwa kwamba wanaongozwa na nguvu ya Mungu, nasi tutambue kwamba ni
kwa namna hiyo hiyo tunavyoongozwa na nguvu ya Mwenyezi Mungu katika maisha
yetu. Sisi tuwe tayari kuiruhusu nguvu ya Mungu ituongoze. Tuiruhusu ituongoze
kila tuamkapo asubuhi, kila tunapotaka kufanya kazi au shughuli yoyote. Ukweli
ni kwamba duniani vipo vikwazo vingi. Yupo shetani anayeleta visirani, wapo
wenzetu wenye hasira na nia mbaya nasi, pia udhaifu wetu katika kufanya mambo
ni mkubwa. Kuna wakati tunapatwa na vitu kama homa, woga na hasira na tunaweza
kufanya mambo ya ajabu kabisa maishani, mambo ambayo hutuharibia kwa kiasi
kikubwa. Lazima tuwe na utayari wa kuikaribisha nguvu ya Mungu ndani ya maisha
yetu ili ituongoze kwa maisha yetu yote.
Katika somo la injili,
Yesu anasisitiza kwamba ufalme wa mbinguni unafanana na juya lililotupwa
baharini likakusanya samaki wa kila aina. Mfano huu waonesha utayari wa Mungu
wa kuwavumilia wenye dhambi. Yupo tayari kutukubali katika udhaifu wetu, na
kutuvumilia tuendelee kufanya kazi naye licha ya udhaifu wetu. Lakini anataka
tusiendelee na udhaifu huu hadi mwisho, anataka tubadilike. Hizi ndizo sababu
za kuwaacha wenye dhambi na wabaya waendelee kuishi pamoja kwa kila wakati.
Tuwe tayari kukubali kubadilika. Tumsifu Yesu Kristo.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment