MASOMO YA MISA, JULAI 27,
2021
JUMANNE, JUMA LA 17 LA
MWAKA
SOMO 1
Kut. 33:7-11; 34:5-9, 28
Desturi ya Musa, ilikuwa
kuitwaa ile hema, na kuikita nje ya marago mbali na hayo marago; akaiita, Hema
ya kukutania. Hata kila mtu aliyekuwa akitaka neno kwa Bwana, akatoka, akaenda
hata hema ya kukutania, iliyokuwa nje ya marago. Hata Musa alipotoka kuiendea
ile hema, watu wote waliondoka wakasimama, kila mtu mlangoni pa hema yake,
akamtazama Musa, hata alipokwisha kuingia hemani. Ikawa Musa alipoingia humo
hemani, ile nguzo ya wingu ikashuka, ikasimama mlangoni pa ile hema; naye Bwana
akasema na Musa. Watu wote wakaiona nguzo ya wingu ikisimama penye mlango wa
hema; watu wote wakaondoka wakasujudu, kila mtu mlangoni pa hema yake.
Naye Bwana akasema na
Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka
akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni
kijana, hakutoka mle hemani.
Bwana akashuka ndani ya
lile wingu, kasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la Bwana. Bwana
akapita mbele yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu wmingi wa huruma, mwenye
fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea
huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhami; wala si mwenye
kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa
baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne. Musa
akafanya haraka, akainamisha kichwa chake hata nchi, akasujudu. Akasema, Ikiwa
sasa nimepata neema mbele zako, Bwana, nakuomba, Bwana, uende kati yetu, maana
ni watu wenye shingo ngumu; ukasamehe uovu wetu na dhambi yetu, ukatutwae tuwe
urithi wako.
Naye alikuwa pamoja na
Bwana siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye
akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi.
Neno la Bwana...
Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 103:6-13 (K) 8
(K) Bwana amejaa huruma
na neema.
Bwana ndiye afanyaye
mambo ya haki,
Na hukumu kwa wote
wanaoonewa.
Alimjulisha Musa njia
yake,
Wana wa Israeli matendo
yake. (K)
Bwana amejaa huruma na
neema,
Haoni hasira upesi, ni
mwingi wa fadhili.
Yeye hatateta siku zote,
Wala hatashika hasira
yake milele. (K)
Hakututenda sawasawa na
hatia zetu,
Wala hakutulipa kwa
kadiri ya maovu yetu.
Maana mbingu zilivyoinuka
juu ya nchi,
Kadiri ileile rehema zake
ni kuu kwa wamchao. (K)
SHANGILIO
2Tim. 1:10
Aleluya, aleluya,
Mwokozi wetu Yesu Kristu
alibatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika kwa Injili
Aleluya.
INJILI
Mt. 13:36 – 43
Yesu aliwaaga makutano,
akaingia nyumbani; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa
magugu ya kondeni. Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa
Adamu; lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale
magugu ni wana wa yule mwovu; yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni
mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika. Basi, kama vile magugu
yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia.
Mwana wa Adamu atawatuma malaika wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na
kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo
wenye haki watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na
asikie.
Neno la Bwana... Sifa
kwako Ee Kristo.
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment