“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumanne Julai 27, 2021
Juma la 17 la Mwaka
Kut 33:7-11;34:5-9.28
Zab 103: 6-13 (k) 8
Mt 13:36-43
KUKUWA KATIKATI YA MAGUGU
Ndugu zangu wapendwa,
karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Katika tafakari yetu ya
neno la Bwana, leo tunakutana na habari kuhusu hema la kukutania. Hapa palikuwa
sehemu maalumu kwa ajili ya kukutania na Bwana kwa wana wa Israeli. Sehemu hii
ilitengwa, iliwekwa sehemu ya pekee, sehemu ya utulivu, na waliingia tu watu
maalumu, mbali na zile sehemu ambazo ni nje ya makazi ya watu ya mara kwa mara,
makazi yasiyokuwa na heshima. Kufanya hivi kulionesha utakatifu na ukuu wa
Mungu, kwamba Mungu ni mkuu, atengewe mahali patakatifu, na mahali palipo na
utulivu.
Pale walipoonesha imani
hii, Bwana alikuja na kufanya makao kati yao, na kusikiliza maombi yao, na
vizazi vijavyo viliweza kujifunza mambo mazuri na kujua zaidi kuhusu ukuu wa
Mungu. Sisi nasi tunapaswa kuheshimu sehemu zetu takatifu, zijengwe mahali pa
utulivu, zitengewe watu maalumu wa kuyatunza. Yapo maeneo ambapo makanisa
yanafanyiwa usafi na kampuni, kampuni zenye watu wasio hata na imani ya
Kikristo. Kwa upande mwingine hapa ni kukosea. Kanisa letu ni nyumba ya
kukutania na Bwana, hata yule anayekuja kufanya usafi ndani yake awe na
heshima, sehemu yako ya ibada lazima uiheshimu, vifaa vyako vya ibada lazima
uviheshimu na uvitunze vyema. Ukianza kuvitapanya tu, mwishowe utashindwa kuona
umuhimu wake. Wengi wetu hatuoni umuhimu wa rozari, misalaba, au sanamu kwa
sababu ya kuvikosea heshima. Tuvitunze vifaa hivi.
Katika somo la injili,
Yesu anaelezea kwamba ibilisi ndiye aliyepanda magugu ndani ya shamba la Bwana.
Magugu haya ni nguvu ya uovu ambayo hadi sasa imekuwa ikiusumbua ulimwengu na
mwanadamu anaishi kati ya nguvu hii ya uovu na wema. Sisi tutambue uwepo wa
watu wa namna hii, watu wenye kupanda uovu na kusia mbegu ya chuki kwenye
maisha yetu. Hawa ni wakala wa ibilisi, watakuwa wanasia mbegu hizi hadi mwisho
wa maisha yetu lakini yafaa tuwe tayari kuzitambua mbegu hizi na kuziepuka ili
zisichafue maisha yetu. Tumsifu Yesu Kristo
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment