MASOMO YA MISA, JULAI 22,
2021
ALHAMISI, JUMA LA 16 LA
MWAKA
SIKUKUU YA MT. MARIA
MAGDALENA
SOMO 1
Wim. 3 :1-4
Usiku kitandani
nalimtafuta mpendwa wa nafsi yangu, Nalimtafuta, nisimpate. Nikasema, Haya,
niondoke nizunguke mjini, Katika njia zake na viwanjani, Nimtafute mpendwa wa
nafsi yangu. Nikamtafuta, nisimpate. Walinzi wazungukao mjini waliniona; Je!
mmemwona mpendwa wa nafsi yangu? Kitambo kidogo tu nikiisha kuwaondokea,
Nikamwona mpendwa wa nafsi yangu.
Neno la
Mungu...Tumshukuru Mungu
Au
SOMO 1
2 Kor. 5 :14-17
Upendo wa Kristo
watubidisha; maana tumehukumu hivi, ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote,
basi walikufa wote; tena alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai
tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa
akafufuka kwa ajili yao.
Hata imekuwa, sisi tangu
sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo
kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena, Hata imekuwa, mtu akiwa
ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! yamekuwa mapya.
Neno la
Mungu...Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATIKATI
Zab 63: 1-5, 7-8 (K) 1
(K) Nafsi yangu inakuonea
kiu, Ee Bwana.
Ee Mungu, Mungu wangu,
nitakutafuta mapema,
Nafsi yangu inakuonea
kiu,
Mwili wangu wakuonea
shauku,
Katika nchi kame na
uchovu, isiyo na maji. (K)
Ndivyo nilivyokutazama
katika patakatifu,
Nizione nguvu zako na
utukufu wako.
Maana fadhili zako ni
njema kuliko uhai;
Midomo yangu itakusifu.
(K)
Ndivyo nitakavyokubariki
maadamu ni hai;
Kwa jina lako nitaiinua
mikono yangu.
Nafsi yangu itakinai kama
kushiba mafuta na vinono;
Kinywa changu kitakusifu
kwa midomo ya furaha. (K)
Maana Wewe umekuwa msaada
wangu,
Na uvulini mwa mbawa zako
nitashangilia.
Nafsi yangu inakuandama
sana;
Mkono wako wa kuume
unanitegemeza. (K)
SHANGILIO
Aleluya, aleluya, Maria
tuambie: sema uliyoona njiani. Kaburi lilimfadhi yule aliye Mzima; Niliona
utukufu wa Kristu alipokuwa akifufuka. Aleluya.
INJILI
Yn. 20 :1-2, 11-18
Siku ya kwanza ya juma
Mariamu Magdalena alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado; akaliona lile
jiwe limeondolewa kaburini. Basi akaenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa
yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, wamemwondoa Bwana
kaburini, wala hatujui walikomweka
Lakini Mariamu alikuwa
akisimama karibu na kaburi, nje yake, analia. Basi akilia hivi, aliinama na
kuchungulia ndani ya kaburi. Akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe,
wameketi, mmoja kichwani na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu. Nao
wakamwambia, Mama, unalilia nini? Akawaambia, Kwa sababu wamemwondoa Bwana
wangu, wala mimi sijui walikomweka. Naye akiisha kusema hayo, akageuka nyuma,
akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu. Yesu akamwambia, Mama unalilia
nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani,
akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami
nitamwondoa. Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania,
Raboni! (yaani, Mwalimu wangu). Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa
kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa
Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu. Mariamu
Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na
ya kwamba amemwambia hayo.
Neno la Bwana... Sifa
kwako Ee Kristo
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment