MASOMO YA MISA,
IJUMAA, JULAI 23, 2021
JUMA LA 16 LA MWAKA
SOMO 1
Kut 20: 1-17
Mungu alinena maneno haya
yote akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri,
katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu ila mimi. Usijifanyie sanamu ya
kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini
duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa
kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya
baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu
maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.
Usilitaje bure jina la
Bwanu, mungu wako, maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina
lake bure. Ikumbuke siku ya sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo
yako yote; lakini siku ya saba ni sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo
usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa
wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya
malango yako. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari,
na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya
sabato akaitakasa.
Waheshimu baba yako na
mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana. Mungu
wako. Usiue. Usizini. Usiibe. Usimshuhudie jirani yako uongo. Usiitamani nyumba
ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi
wake, wala ng’ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani
yako.
Neno la
Mungu...Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 19:8-11 (K) Yn. 6:68
(K) Bwana, unayo maneno
ya uzima wa milele.
Sheria ya Bwana ni
kamilifu huiburudisha nafsi
Ushuhuda wa Bwana ni
amini humtia mjinga hekima. (K)
Maagizo ya Bwana ni
adili, huufurahisha moyo,
Amri ya Bwana ni safi,
huyatia macho nuru. (K)
Kicho cha Bwana ni
kitakatifu, kinadumu milele.
hukumu za Bwana ni kweli,
zina haki kabisa. (K)
Ni za kutamanika kuliko
dhahabu,
kuliko wingi wa dhahabu
safi.
Nazo ni tamu kuliko
asali, kuliko sega la asali. (K)
SHANGILIO
Mt. 4:4
Aleluya, aleluya,
Mtu hataishi kwa mkate
tu,
ila kwa kila neno
litokalo
katika kinywa cha Mungu
Aleluya.
INJILI
Mt. 13:18-23
Yesu aliwaambia wanafunzi
wake: Ninyi sikilizeni mfano wa mpanzi. Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe
nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye
aliyepandwa karibu na njia. Naye aliyepandwa penye miamba. huyo ndiye
alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; lakini hana mizizi ndani
yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno,
mara huchukizwa. Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno;
na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa
halizai. Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno,
na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu
thelathini.
Neno la Bwana... Sifa
kwako Ee Kristo.
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment