MASOMO YA MISA,
IJUMAA, JULAI 16, 2021
JUMA LA 15 LA MWAKA
SOMO 1
Kut. 11:10-12:14
Musa na Haruni walifanya
ajabu hizo zote mbele ya Farao; Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu,
asiwape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake.
Bwana akanena na Musa na
Haruni katika nchi ya Misri, akawaambia, Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi
kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu. Semeni na mkutano wote wa
Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwanakondoo,
kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwanakondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa
watu wa nyumba ni wachache kwa mwanakondoo, basi yeye na jirani yake aliye
karibu na nyumba yake na watwae mwanakondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya
watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa
yule mwanakondoo. Mwanakondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa
katika kondoo au katika mbuzi.
Nanyi mtamweka hata siku
ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli
watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kutia katika miimo
miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. Watakula
nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena
pamoja na mboga zenye uchungu. Msiile mbichi wala ya kutokoswa majini, bali
imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na nyama zake za ndani. Wala
msisaze kitu chake chochote hata asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi
mtakichoma kwa moto. Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa
viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni
pasaka ya Bwana.
Maana nitapita kati ya
nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya
Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya
Misri; Mimi ndimi Bwana. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika ile damu,
nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lolote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya
Misri.
Na siku hii itakuwa
ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu
katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele.
Neno la Bwana… Tumshukuru
Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 116:12-13, 15-18 (K)
13
(K) nitakipokea kikombe
cha wokovu,
na kulitangaza jina la
Bwana.
Nimrudishie Bwana nini
Kwa ukarimu wake wote
alionitendea?
Nitakipokea kikombe cha
wokovu;
Na kulitangaza jina la
Bwana. (K)
Ina thamani machoni pa
Bwana
Mauti ya wacha Mungu
wake.
Ee Bwana, hakika mimi ni
mtumishi wako,
Umevifunga vifungo
vyangu. (K)
Nitakutolea dhabihu ya
kushukuru;
Na kulitangaza jina la
Bwana;
Nitaziondoa nadhiri zangu
kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake
wote. (K)
SHANGILIO
Zab. 119:28, 33
Aleluya, aleluya,
Unitie nguvu sawasawa na
neno lako,
ee Bwana, unifundishe
njia ya amri zako.
Aleluya.
INJILI
Mt. 12:1 – 8
Wakati ule Yesu alipita
katika mashamba siku ya sabato; wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kuvunja
masuke, wakala. Na Mafarisayo walipoona, walimwambia, Tazama! Wanafunzi wako
wanafanya neno ambalo si halali kulifanya siku ya sabato.
Akawaambia, Hamkusoma
alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? Jinsi alivyoingia katika
nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila
wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika torati,
kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? Lakini
nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu. Lakini kama mngalijua
maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na
hatia. Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.
Neno la Bwana… Sifa kwako
Ee Kristo.
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment