*“ASALI ITOKAYO
MWAMBANI”*
Tafakari ya kila siku
Ijumaa, Julai 16, 2021,
Juma la 15 la Mwaka
Kut 11:10 – 12:14;
Zab 116:12-13, 15-18;
Mt 12:1-8
*KUSHIKA SIKU TAKATIFU YA
SABATO!*
Karibuni sana ndugu
wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo katika tafakari
yetu ya Neno la Bwana, katika somo la kwanza, tunasikia juu ya ishara na
maajabu aliyoyatumia Mwenyezi Mungu kusaidia kuwaondoa wana wa Israeli nchini
Misri. Walipewa maagizo ya namna ya kufanya: ilibidi kumchinja Mwanakondoo na
damu yake kupakwa juu ya miimo na vizingiti vya nyumba yao na kwa nguvu ya damu
hii, waliweza kuokoka toka katika maangamizi ya yule malaika wa kifo
aliyewaangamiza Wamisri. Ukisoma Kut 12:37, utagundua kwamba wapo ambao
hawakuwa waisraeli ambao nao walikubali nyumba zao zipakwe hii damu na hakika
waliweza kuokoka.
Twaweza kujiuliza, je hii
damu ilikuwa ya namna gani? Ilikuwa na nguvu za namna gani? Hakika haikuwa tu
na nguvu za damu ya mbuzi au kondoo wa kawaida bali ilikuwa na nguvu zaidi. Na
nguvu hii ilipata toka kwa Mungu Mwenyewe. Na uwezo wa damu hii ulizidi
kuonekana hata pale walipokuwa wanavuka bahari ya shamu. Ni wale tu
walioshiriki katika kumla yule mwana kondoo na nyumba zao kupakwa hii damu ndio
tu walioweza kuvuka. Wasiokuwa na hii damu waliishia kufa maji, walishindwa
kuvuka kwenda upande wa pili.
Hakika damu hii ina nguvu
ya pekee. Damu hii yaashiria ukuu wa damu ya Yesu. Hadi leo yeyote asiyefunikwa
na damu hii hupotea, atashambuliwa na malaika wa mauti, na pia atashindwa
kuvuka kwenda katika upande wa pili wa bahari yaani kwenye nchi ya ahadi
mbinguni.
Sisi tuziheshimu sakramenti
zetu. Tuepuke madharau. Hakika kwa macho zinaonekana kuwa ishara tu, lakini
ndani yake zina neema kubwa, "supernatural grace".
Katika somo la injili,
Yesu anafundisha kwamba Sabato iliwekwa ili imsaidie mwanadamu, aupate wokovu;
na si ituletee chuki kati yetu. Kinachojenga ni upendo. Hata kama ni kwenye
kushika sheria za Mungu, tuwe tayari kuangalia mazingira. Tusihukumu mtu fulani
bila kuangalia nini kilichotokea, 'stress' alizokuwa nazo na mambo mengine
mengi.
Tuwe na utayari wa namna
hii ndugu zangu. tuache kufuata sheria bila kuonesha upendo. Tumsifu Yesu
Kristo.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment