“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumanne, Julai 20, 2021,
Juma la 16 la Mwaka wa
Kanisa
Kut 14:21-15:1;
Zab 15: 8-10,12,17;
Mt 12: 46-50
MAPENZI YA MUNGU!
Karibuni sana wapendwa wa
Bwana kwa adhimisho la Misa takatifu asubuhi ya leo. Tafakari yetu ya neno la
Mungu katika somo la kwanza tunasikia habari za wana wa Israeli kufanikiwa
kuvuka katika bahari ya shamu. Kuvuka bahari ya shamu ilikuwa miongoni mwa
matukio makuu yaliyoifanya Israeli ishangae, hadi imwimbie Bwana wimbo wa
shukrani kwa sababu ya jinsi walivyouona ukuu na nguvu ya Mungu ikifanya kazi
kati yao.
Katika kuvuka bahari hii,
yapo makundi mawili ya watu. Wapo kwanza wamisri ambao walikuwa wanawakimbiza
wana wa Israeli na wapo pia wana wa Israeli waliokuwa wametoka utumwani Misri.
Wote wanaingia katika bahari moja baada ya maji kugawanyika. Cha ajabu ni
kwamba baada ya muda sio mrefu, mgawanyiko unatokea. Maji yalirudi na cha
ajabu, yale maji yakaleta utengano, yaliwauwa wale Wamisri, wale ambao
hawakushiriki katika kumla mwanakondoo na kuwaacha waisraeli, wale ambao
walishiriki katika kumla yule mwanakondoo.
Hivyo nguvu ya damu ya
Mwanakondoo ilikuwa ikifanya kazi ndani yao. Tukio hili linaashiria pia maisha
yajayo-kwamba kwa nguvu ya sakramenti tuzipewazo za kanisa, hakika tutaweza
kuvuka na kufikia mbinguni. Wamisri walikosa kinga ya yule mwanakondoo na ndio
maana walikufa maji. Wana wa Israeli walikuwa na nguvu, kinga ya yule
mwanakondoo, damu yake ilikuwa bado na nguvu ya kuwalinda na ndio maana
hawakuweza kufa maji. Sisi tuzidi kuziheshimu sakramenti hizi. Zitatuwezesha
kuvuka na kufikia upande wa pili wa bahari yaaani mbinguni.
Katika somo la injili,
Yesu anamtangaza yeyote yule anayetii mahusia yake ndiye baba na mama yake. Kwa
kusema hivi, Yesu anajitangaza kuwa rafiki na ndugu wa yeyote. Hivyo kuyashika
maagizo ya Yesu ni jambo la muhimu. Hili linatutangaza, linatutambulisha kuwa
kaka na dada wa Yesu. Kuwa kaka na dada wa Yesu ni thamani kubwa.
Hii ni ashirio la uwepo
wa uhusiano mkuu, uhusiano wenye kutuletea mema. Hivyo tutambue kwamba matendo
mema huimarisha uhusiano wetu na Mwenyezi Mungu. Hili litutie moyo katika
kutenda matendo mema. Kila jema tulitendalo ni hazina kwetu kwani hakuna
kinachopotea. Wema hauozi, kama huoni faida yake kwa sasa, utaipata baadaye.
Tusiache kutenda mema. Mema yetu yatatutetea. Bwana unisaidie nipate moyo wa
kutenda mema.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment