"ASALI ITOKAYO
MWAMBANI"
Tafakari ya kila siku
Ijumaa, Julai 9, 2021,
Juma la 14 la Mwaka
Mwa 46:1-7, 28-30;
Zab 36:3-4, 18-19, 27-28,
39-40;
Mt 10: 16-23
KONDOO NA MBWA MWITU!
Karibuni sana ndugu zangu
wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Katika tafakari yetu ya
neno la Bwana, katika zaburi yetu ya wimbo wa katikati, tunakutana na maneno
yasemayo kwamba wokovu wa wenye haki u na Bwana. Maneno haya ya zaburi
yanatumika kutilia mkazo ujumbe wa somo la kwanza ambapo Yakobo na familia yake
yote inapata kuokolewa kutoka katika njaa iliyokuwa inalikabili taifa la
Kanaani. Analetwa Misri na kuufanya uhai wake uokoke; yeye na familia yake.
Hakika wokovu wa wenye haki u na Bwana kwani tukijaribu kuangalia namna jinsi
huu wokovu ulivyoletwa, hadi Yakobo na uzao wake unakuja kuokolewa na njaa
hakika inashangaza.
Hapa ndio tunapoweza
kuona mkono wa Mungu katika tukio hili. Kumbe tukio tulilolidhania kwamba ni la
kikatili, limegeuka kuwa tukio la kuleta neema kwa familia nzima. Hakika Mungu
ana mipango mingi ajabu. Yeye aweza hata kugeuza ugumu wetu kuwa furaha. Hivyo
tusilalamike sana kwa wale ambao tumewahi kutendewa ukatili na wenzetu,
usilalamike. Ni kumwomba Mungu alete mema ndani ya huo unyama uliokwishatendewa
kama ilivyotokea kwa Yusufu.
Usibakie katika
kulalamika na kukata tamaa. Tambua kwamba Mwenyezi Mungu aweza kubadili ubaya
uliotendewa kuwa uzuri wenye kuleta furaha ya ajabu.
Katika somo la injili,
Bwana Yesu anawaeleza wanafunzi wake waziwazi kwamba wajihadhari na wanadamu.
Wanadamu wanaelezwa kama kikwazo chao cha kwanza kwao. Hawa ndio
watakaowapeleka katika masinagogi na kuwafanya wachapwe viboko. Lakini wanatiwa
moyo na Yesu leo. Wanaagizwa kwamba wakifukuzwa katika mji huu, waende mji
mwingine. Wasikate tamaa kwa kufukuzwa katika eneo moja. Haimaanishi kwamba
watakataliwa na wote, wapo watakaowapokea.
Hili liwe fundisho kwetu
ndugu zangu. Tukikataliwa katika eneo mojawapo au ukikatishwa tamaa na mtu
mmojwapo, jaribu pia mwingine. Haimaanishi kwamba wewe utakataliwa na wote.
Hili litutie matumaini hasa katika kuihubiri injili. Injili imerudi nyuma kwani
watu tunakatishwa tamaa kirahisi mno. Hatuna utayari wa kusema kwamba
tukikataliwa eneo moja, twende jingine. Wapo tunaofikiri kwamba ukikataliwa na
mmoja basi kwa wengine itakuwa hivyo hivyo. Hii ni mbinu shetani anayotumia
kuirudisha nyuma injili au kutufanya tushindwe kufanya maridhiano ndani ya
jumuiya zetu. Hivyo njia moja ikishindwa, jaribu nyingine. Kwa namna hiyo utafanikiwa
kuleta maridhiano katika jamii, utaweza kutatua mengi ndani ya jamii na kufanya
pia injili isonge mbele. Ukichukiwa na mtu mmoja usidhani dunia yote
inakuchukia. Wapo wanaokupenda. Tumsifu Yesu Kristo.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment