“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumatano, Juni 30, 2021.
Juma la 13 la Mwaka
Mwa 21: 5, 8-20;
Zab 34: 7-8, 10-13;
Mt 8: 28-34
UTUOPOE MAOVUNI!
Watu waliokuwa na pepo
wakitokea makaburini walikutana na Yesu wakati Yesu akikaribia kijiji hicho.
Walikuwa wakali mno kiasi kwamba hakuna mtu aliye jaribu kupita katika njia
ile. Walilia kwa sauti “una nini nasi, Mwana wa Mungu?” sehemu hii inaonesha
kwamba pepo ni hatarishi na kwamba Yesu ana mamlaka makubwa. Yesu anaingia
mjini kwa kuwaponya hawa watu wawili waliokuwa na pepo na hivyo kuonesha nguvu
yake juu ya kuondoa uovu.
Ni wazi kwamba hawa pepo
waliowashika hawa watu wawili walikuwa wakali na hivyo kufanya watu wakae kwa
hofu na wasi wasi. Watu kuwa na wasiwasi kiasi kwamba hakuna mtu aliye thubutu
kupita maeneo hayo. Tunaweza tusikutane na uovu kama huo mara kwa mara, lakini
ni hakika kwamba tulisha kutana na uovu wakati mwingine. Muovu yupo daima na anazunguka
kutafuta sehemu ya kujenga ufalme wake hapa duniani. Yesu ana mamlaka makubwa
kuliko muovu. Jambo lakushangaza, aliwatoa pepo hawa na wakawaingia kundi kubwa
la nguruwe na hivyo kuteremkia baharini na kufa. Watu wa mji ule wanaogopa
kiasi cha kumwambia Yesu aondoke katika mji wao. Kwa kiasi, sababu inaonekana
Yesu kuwaponya hawa watu wawili ilileta mtafaruku mkubwa sana katika mji. Uovu
uliojikita hauondoki kimya kimya. Kuna mahangaiko!
Watu hawa wawili walitoka
makaburini , kama sisi tunavyotoka katika makaburi ya dhambi-tuliko naswa,
anasa, kuhukumu kwetu wengine, dhuluma, na mitazamo yetu mibaya kwa wengine
inayoleta maumivu kwa wengine. Kwasababu ya hili watu wanaweza kutuogopa sana!
Lakini Yesu yupo tayari kuja kukutana na sisi sehesmu tulipo. Uovu wetu
humtambua Yesu na tunafanywa kuwa huru kama tukienda karibu na Yesu.
Lakini mara nyingi, Yesu
anapokuja kuondoa uovu ndani mwetu, tunaweza tusitambue uponyaji. Ni mara ngapi
Roho Mtakatifu anataka kutufanya upya nasi tunakataa? Tuna furaha kuishi katika
hali ya dhambi na hatutaki kuacha. Hatutaki mtu atusumbue tunapo endelea
kufurahia raha za ulimwengu. Tutafakari juu ya maisha yetu na kujaribu kuwa
tayari katika maongozi ya Mungu na wala tusimuombe aondoke kama wale watu
kwenye Injili, ili tupate kuishi katika maisha ya neema tele.
Sala: Bwana, nisaidie
niweze kubaki imara ninapo kumbana na muovu na utawala wake wa giza. Nisaidie
niweze kushinda utawala wake kwa ujasiri, upendo na ukweli ili kuleta ufalme
wako sehemu yake. Yesu nakuamini wewe. Amina.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment