“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumanee, Juni, 29, 2021,
Juma la 12 la mwaka wa
Kanisa.
Sherehe ya Watakatifu
Petro na Paulo Mitume
Mdo 12:1-11;
Zab 33:2-9;
2Tim 4:6-8, 17-18;
Mt 16:13-19
MATESO YETU YA KILA SIKU
YANATUSAIDIA KUKUWA KATIKA UHUSIANO NA YESU!
Karibuni ndugu zangu
kwenye tafakari ya neno la Mungu siku ya leo tunapoadhimisha sherehe ya watakatifu
Petro na Paulo. Hii ni miamba mikubwa ya kanisa iliyolisaidia sana Kanisa.
Walitumia muda, akili na uhai wao kwa ajili ya Kristo. Kwao, kuishi ilikuwa ni
Kristo na hata kufa ilikuwa ni faida. Na hili walilidhirisha kwenye maisha yao.
Kweli walikuwa watu wa imani na Mungu aliwasaidia sana kwenye utume wao huu kwa
kanisa na hili linadhihirishwa katika masomo yetu ya leo.
Katika zaburi ya wimbo
wetu wa katikati leo, tunakutana na mzaburi anasali akionesha Imani kubwa kwa
Mungu kwamba kamwe hataacha kumtukuza na kumheshimu Bwana na anawaalika watu
wamtukuze Bwana pamoja naye kwani Bwana amekuwa mwema kwake kila wakati kwani
aliwahi hata kumtuma malaika wake akamuokoa kwenye hatari na kumfanya asiabike
mbele ya maadui wake. Jambo hili linamfanya asiache kuyatangaza matendo makuu
ya Mungu na anaahidi kwamba kamwe hataacha kuzitamka sifa za huyu mwenyezi
Mungu kwa msaada wake huu.
Kwenye masomo yetu ya
leo, miongoni mwa watu waliokutana na msaada kama huu ni Petro mtume ambaye
kwenye somo la kwanza, habari hii inaelezewa, jinsi Mungu alivyomuokoa mikononi
mwa adui katili kabisa-Herode, aliyetaka kumnyonga mbele ya watu. Petro
alimshukuru Mungu sana kwa hili tukio na alitambua kwamba ni malaika wa Bwana
ametumwa ili kumwokoa. Mtume Paulo naye aliokolewa kwenye matukio makubwa na
malaika. Yeye alipotaka kuuawa kule mjini Dameski, alitelemshwa nje ya mji
kupitia kapu. Hapa napo ni malaika tu aliyetumwa ili kumwokoa.
Ndugu zangu, mitume hawa
walipewa ulinzi wa hali ya juu na Mungu kwani pia walikuwa mihimili mikubwa kwa
kanisa. Yesu asingaliruhusu wafe kabla ya wao kutimiza ule utume wao na
waliache kanisa kwenye hali nzuri. Wao walijitoa mno kwa ajili ya Mungu na
Mungu alijitoa kwa ajili ya kuwalinda. Nasi ndugu zangu tusiache kujitoa kwa
ajili ya kazi ya Mungu. Kama sisi ni mapadre, masista, makatekista, watawa,
waamini tujitoe kwa ajili ya kazi ya Mungu. Kazi yake tuiweke mstari wa mbele.
Kama ni padre-tutambue kwamba utume kwa ajili ya watu wa Mungu ndio cha
kwanza-fanya hivi naye Mungu atatubariki. Tukijidai kuhangaikia maslahi
nakueleza hatutavuna chochote. Kwa mwanzoni tutafikiria labda tunavuna pesa
lakini baadaye kumbe tutajiona kwamba kweli hatujafanikiwa kwenye chochote.
Hata zile mali ulizojidai kutumia muda wote kuzianzisha itafika mahali ziishe
kama hewa-au mtu atakudhulumu na utaishia kujiona kana kwamba kazi zako zote ni
bure. Wote walioacha kazi ya Bwana na kuishia kwenye kujitafutia maslahi,
wameishia tu kuanzisha vitu vilivyokuja kuishia kwenye kudhulumiwa na wenzao.
Hivyo jamani tuithamini kazi ya Bwana. Tuiweke iwe mbele kabisa. Kazi ya Bwana
itakutunza tu, itakufanya upate ulinzi kama Petro na Paulo walivyopatiwa. Mungu
atatuepusha na magonjwa mbalimbali na ajali za namna mbalimbali kwasababu sisi
ni watumishi wake na tunaithamini kazi yake. Hivyo, Mungu atakupatia ulinzi na
upendeleo wa pekee. Fanya hivi ndugu yangu na kweli tutatambua ukweli wa jambo
hili. Awe padre, awe katekista, sista, mwenyekiti jumuiya-wewe fanya hivi, ipe
kazi ya Bwana nafasi ya kwanza kama haitakutunza. Wewe fanya hivi na hakika
utaona tu. Mimi nasema kile nilichowahi kukiona maishani.
Katika somo la injili,
tunakutana na Petro akimkiri kwamba Yesu ni Masiha. Petro alikuwa wa kwanza
miongoni mwa mitume kutambua hili kwa hekima na uwezo wa hali ya juu sana.
Paulo naye alilionyesha hili kwamba anamkiri Yesu kama Masiha katika nyaraka
zake mbalimbali. Nasi kama Petro na Paulo tumkiri Yesu wetu kama Masiha. Hakika
atatulinda tu na kamwe hatatuacha. Tumkiri huyu Yesu, tusimuache, jitoe kwa
ajili ya Yesu naye atajitoa kwa ajili yako. Ukijitoa kwa ajili yake atakulinda
tu hata kuacha. Atakuokoa. Hawezi kukuacha bila ulinzi. Tafakari hii jamani
iwafikie wakristo wote-na tujitoe zaidi kwa kazi ya Kanisa tukisukumwa na
tafakari hii. Tukiambiwa kwamba kuna kazi ya kupamba kanisani au kudeki
kanisani, tuwe wa kwanza kukimbilia-pale ndio penye neema jamani. Tusiache
hivi.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment