MASOMO YA MISA, JUNI 7,
2021
JUMATATU , JUMA LA 10 LA MWAKA
SOMO 1
2Kor. 1:1-7
Paulo, mtume wa Kristo
Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu; kwa kanisa la Mungu lililoko
Korintho, pamoja na watakatifu wote walioko katika nchi yote ya Akaya. Neema na
iwe kwenu na Amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
Na ahimidiwe Mungu, Baba
wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote; atufarijiye katika
dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna
zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu. Kwa kuwa kama vile mateso ya
Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa njia ya Kristo.
Lakini ikiwa sisi tu katika dhiki, ni kwa ajili ya faraja yenu na wokovu wenu;
au ikiwa twafarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu; ambayo hutenda kazi yake kwa
kustahimili mateso yale tuteswayo na sisi. Na tumaini letu kwa ajili yenu ni
imara, tukijua ya kuwa kama vile mlivyo washiriki wa yale mateso, vivyo hivyo
mmekuwa washiriki wa zile faraja.
Neno la Bwana… Tumshukuru
Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 34:1 – 8 (K) 8
(K) Onjeni mwone ya kuwa
Bwana yu mwema
Nitamhimidi Bwana kila
wakati,
Sifa zake zi kinywani
mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu
itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie
wakafurahi. (K)
Mtukuzeni Bwana pamoja
nami,
Na tuliadhimishe jina
lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana
akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu
zote. (K)
Wakamwelekea macho
wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona
haya.
Maskini huyu aliita,
Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake
zote. (K)
Malaika wa Bwana hufanya
kituo,
Akiwazungukia wamchao na
kuwaokoa.
Onjeni mwone ya kuwa
Bwana yu mwema;
Heri mtu yule
anayemtumaini. (K)
SHANGILIO
Zab. 119:18
Aleluya, aleluya,
Unifumbue macho yangu
niyatazame, maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya.
INJILI
Mt. 5: 1-12
Yesu alipowaona makutano,
alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; akafumbua
kinywa chake, akawafundisha, akisema, Heri walio maskini war oho; maana ufalme
wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; maana hao watafarijika. Heri wenye upole;
maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki; maana hao
watashibishwa. Heri wenye rehema; maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo
safi; maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi; maana hao wataitwa wana wa
Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo,
kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa
mbinguni, kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.
Neno la Bwana…. Sifa
kwako Ee Kristo
-------------------------
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see
www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment