“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumatatu, Juni 7, 2021.
Juma la 10 la Mwaka
2 Kor 1: 1-7;
Zab 34: 2-9;
Mt 5: 1-12
HERI WALIO…..!
Karibuni sana ndugu
wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha
kumbukumbu ya Bikira Maria mama wa Kanisa. Ni kumbukumbu iliyoamriwa
iadhimishwe baada ya Pentecoste kuonesha ushirika na mchango wa Maria katika
Kanisa.
Roho Mtakatifu
aliwashukia mitume na wafuasi wa kwanza wa Kristo siku ya Pentecoste. Roho
Mtakatifu alikuwa na mchango mkubwa sana katika kuiunda, kuiongoza na kuilinda
hii jamii ya Mwanzo ya Wakristo. Roho aliwaondolea woga, aliwafanya watoke na
kwenda kuhubiri injili kila mahali. Tukisoma katika Matendo ya Mitume 2:41,
tunagundua kwamba kwa nguvu ya Roho, karibu watu elfu tatu waliweza kubatizwa
katika ile siku ya Pentecoste. Hakika Roho alitoa nguvu ya ajabu. Roho alizidi
kuwaongoza, kuwatetea na kulifundisha kanisa.
Roho Mtakatifu amelitetea
kanisa ili lisiangamizwe na Makaisari wakorofi kama akina Nero na Domitian.
Roho Mtakatifu ndiye mwenye kulitakasa kanisa na kulifanya kuwa Israeli mpya na
kwa njia yake tunaweza kumfikia Mwenyezi Mungu wetu-bila Roho Mtakatifu, kanisa
lisingeliweza kuanza na kuwashinda maadui wake.
Mama Maria ni mwenye
nafasi kubwa ndani ya kanisa, ndiye aliyekuwa kiongozi na mshauri wa jamii ya
kwanza ya Wakristo. Pia amekuwa mwombezi wa kanisa baada ya kupalizwa mbinguni.
Nafasi ya Mama Maria katika kanisa ni kubwa sana. Hivyo astahili nafasi ya
pekee katika kanisa. Hivyo tunayo kila sababu ya kumheshimu Maria kama Mama wa
kanisa baada ya Pentecoste.
Katika somo la kwanza
leo, tunasikia juu ya dhambi na uadui uliongia ulimwenguni baada ya dhambi ya
Eva. Eva alionesha ukaidi, hakutii sauti ya Mungu na hivyo kuiletea dunia
madhara makubwa. Mama Maria alionesha utii mkubwa na kwa utii wake aliiletea
dunia ukombozi. Na leo anachaguliwa na Mwanae kuwa Mama wa Wafuasi wake. Mama
Maria aliweza yote haya kwa sababu alionesha utii mkubwa. Kama angeonesha
ukaidi, hakika asingaliweza kuwa wa faida kwetu.
Utii huu wa Mama Maria
ututie moyo na sisi tupate kuwa watii. Utii utatuletea faida kubwa. Pia
utusaidie sisi kukimbilia ulinzi wa Mama Maria kila siku. Kanisa lisimtupe Mama
Maria pembeni kwa wakati wowote. Mama Maria ndiye mwombezi wake. Likimbilie
msaada na maombezi yake kwa kila siku.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment