“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Alhamisi, Juni 10, 2021.
Juma la 10 la Mwaka
2 Kor 3:15 – 4:1,3-6;
Zab 85:9-14;
Mt 5:20-26
KUFANYA MAKAO!
Karibuni sana wapendwa
wangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu inaanza
kwa kuiangalia Zaburi yetu ya wimbo wa katikati. Zaburi hii inatupatia ujumbe
kuhusu Utukufu wa Bwana kukaa kati yetu. Matunda ya utukufu wa Bwana kukaa kati
yetu ni kuwa na amani, furaha na upendo kati yetu. Bwana huwa karibu nasi naye
hutupatia msaada.
Katika Somo la kwanza,
Mt. Paulo anaeleza kwamba Wayahudi waliokataa kumtii Kristo walishindwa
kuukaribisha utukufu wa Mungu uje ukae kati yao. Hivyo walibakia katika upofu,
akili zao zikafunikwa na giza. Giza hili litaondolewa kwa pale watakapomgeukia
Kristo na kuiamini injili yake. Ndugu zangu, Wayahudi wanaelezwa kwamba ipo
faida kubwa ikiwa wataipokea injili. Injili itawaletea ukamilifu. Injili
itawapatia uhuru na kujua namna ya kuenenda kati kati ya ulimwengu huu.
Wakristo wa Mwanzo
waliporuhusu injili iwaongoze, walipata amani kubwa maishani mwao. Japokuwa
walikuwa watu wa kipato cha chini, waliweza kuishi maisha ya uhuru na
kutokutindikiwa. Injili ilimgusa kila mkristo ili aweze kumsaidia mwenzake.
Kila aliyeeleza shida yake aliweza kusaidiwa kwa sababu injili iligusa maisha
yao. Na hivyo walipoelezana shida, walisikilizana. Hivyo kanisa liliweza kukua
sana.
Sisi tuzidi kukazana
kuishi injili yetu. Nyakati zetu, wengi wetu tunapata shida kwa sababu wengi
hatuguswi na injili. Hivyo hata wenzetu wakitueleza shida zao, hatusikilizi.
Yafaa injili itusaidie, tubadilike tena.
Katika somo la injili,
miongoni mwa yanayofundishwa na Yesu ni juu ya kutambua kwamba hawapaswi
kujilinganisha na wafarisayo au wanasheria. Maisha yao ya kimaadili yanapaswa
kuwapita hata ya hawa wafarisayo. Yesu anawataka wawe watu wenye kutoa vitu
vyenye ubora. Hata sadaka zao na sala zao mbele ya Mungu zafaa ziwe bora.
Wazitoe katika moyo safi, baada ya mapatano na wenzao, hapa Mungu atazipoke.
Huu ndio ukristo.
Injili hii iwe fundisho
kwetu ndugu zangu. Mara nyingi, wengi wetu hatukui kimaadili kwa sababu
tunatabia ya kujilinganisha na wenzetu. Tunajilinganisha na wezi, wauaji na
kusema labda sisi ni bora kuliko wao. Na hivyo tunakuwa tayari kusema kwamba
afadhali hata mimi natendaga dhambi ndogo. Wenzangu wanatenda zaidi. Na hivyo
tunahalalisha dhambi zetu na mwishowe tunaanguka kiroho. Hii sio sahihi.
Tunapaswa kujua kwamba
kama ni wema, tuwe na wema wa hali ya juu kabisa. Tuache kuhalalisha dhambi kwa
kujilinganisha na wenzetu. amina.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment