“KUFUFUKA NA KRISTO”
Tafakari ya Pasaka
Jumatatu, Mei 17, 2021.
Juma la 7 la Pasaka
Mdo 19: 1-8;
Zab 67: 2-7 (R. 33);
Yn 16: 29-33.
WAKRISTO WENYE KUTOA
USHUHUDA!
Karibuni sana ndugu zangu
wapendwa kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo katika adhimisho la Misa
Takatifu. Leo neno la Bwana linaanza kwa kulitazama somo la kwanza. Hapa
tunakutana na Mtume Paulo akiwaombea Roho Mtakatifu wafuasi wa Kristo huko
Efeso. Wafuasi hawa walibatizwa na Apolo kwa ubatizo wa toba, wa Yohane
Mbatizaji.
Paulo anawawekea mikono
na kupokea nguvu ya Roho Mtakatifu na kuanza kuongea kwa ndimi. Roho Mtakatifu alihitajika
ili kuwaimarisha wafuasi hawa ndugu zangu. Bila huyu Roho Mtakatifu,
wasingaliweza kuiishi imani yao. Yesu aliwaagiza wafuasi wake kwamba wasijaribu
kutoka Yerusalemu kabla ya kumpokea Roho Mtakatifu. Pale wangejaribu hivyo,
wasingaliweza kumtangaza Kristo, kwanza wangekosa maarifa ya kumtangaza kristo,
halafu wangekosa cha kutangaza, na wangekosa nguvu ya kutangaza. Hivyo,
wangalishindwa kirahisi. Hivyo, ilibidi wampokee Roho Mtakatifu ili waweze
kupokea haya.
Leo Paulo anawaombea Roho
Mtakatifu ili wakristo wa Efeso waweze kuishi imani yao hivi, na kupata cha
kutangaza na kuweza kumtangaza Kristo wetu vyema. Sisi tujifunze kutambua
nafasi ya Roho Mtakatifu maishani mwetu hasa katika imani yetu. Tukijiona
tunatetereka kiimani, tunaanguka kirahisi, tunakuwa waoga, tunakosa hekima ya
kuongoza maisha yetu, tunafungwa na ulevi, uasherati, na fujo-tukiona
haya-lazima tuchunguze uhusiano wetu na Roho Mtakatifu. Tunapaswa kumwalika
Roho atusaidie kwani ndiye atakayetusaidia katika magumu ya namna hii ndugu
zangu.
Yesu katika injili
anatueleza kwamba ulimwenguni tutapata magumu lakini tujipe moyo. Sisi tusiache
kujipa moyo, tuna kila sababu ya kujipa moyo kwani tunaye Roho Mtakatifu.
Hakika atatusaidia. Yesu aliweza kushinda. Nasi tusiache kujikabidhi mikononi
mwa Roho Mtakatifu. Hakika tutashinda. Tuzidi kujiombea wenyewe, tuwaombee na
ndugu zetu na viongozi wetu, ili wazidi kupokea baraka toka kwa Mwenyezi Mungu,
na Roho wa Mungu aongoze mawazo yao na utendaji wao. Tumsifu Yesu Kristo.
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment