“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
Jumanne, Mei 18, 2021,
Juma la 7 la Pasaka
Mdo 20: 17-27;
Zab 68: 10-11, 20-21(K.
33);
Yn 17: 1-11.
UTUME WA KUTIMIZA!
Ndugu wapendwa, karibuni
kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu ya neno la
Bwana itaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na Paulo
akiongea kwa kujiamini kabisa juu ya utume wake huko Efeso. Hakika aliufanya
kwa moyo sana na leo anakamilisha utume huo.
Moyo wa Paulo umeridhika,
Paulo aliruhusu kuongozwa na Roho wa Bwana, alivitumia vipaji vyake vyema na
muda wake aliutumia vizuri. Sisi tuombe kuwa kama Paulo leo. Mara nyingi
tumekuwa watu wa kulalamika baada ya kufanya wajibu zetu kwa sababu ya kuruhusu
uzembe na mizaha kwenye shughuli zetu. Mwisho wa siku tunashindwa kufaulu
vyema. Tujichunguze, namna tunavyotumia vipaji vyetu, na muda wetu. Tusiruhusu
uvivu au matani yaingie ndani yake mnoo. Hizi ndizo sababu za sisi kujilaumu.
Tukishirikiana na Roho
Mtakatifu, hakika hatutakuwa na sababu ya kujilaumu au kujiona kushindwa.
Tutatumia muda wetu na vipaji vyetu vyema. Roho Mtakatifu ndiye msaidizi wetu.
Leo katika siku yetu ya tano ya Novena, tumwombe Roho Mtakatifu atusaidie
katika hili.
Katika somo la injili,
Yesu anadhihirisha dhahiri kwamba hakika ametekeleza utume wake vyema.
Amekamilisha kazi aliyotumwa kutekeleza na Baba. Na sasa anawaombea wanafunzi
wake waitekeleze kazi yake ya utume. Sisi tuwe na moyo wa kuwaombea wenzetu
kama anavyofanya Yesu leo. Mara nyingi baada ya kumaliza wajibu wetu,
hatumuombei yule anayechukua madaraka baada yetu. Wengi wetu tunatabia ya
kupendelea maanguko ya wenzetu, hasa wale wanaochukua baada yetu. Tusiruhusu
tabia hizi za kishetani zitawale kazi ya Bwana, lazima tumwige Yesu.
Kazi ya Bwana inarudishwa
nyuma kwa sababu ya kuruhusu wivu na tabia za kuombeana mabaya katika utume
wetu. Tusiombeane mabaya; tuombeane baraka toka kwa Mwenyezi Mungu. Tumsifu
Yesu Kristo.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment