MASOMO YA MISA, MEI 18,
2021
JUMANNE YA 7 YA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 20 :17-27
Siku zile, toka Mileto
Paulo alituma watu kwenda Efeso, akawaita wazee wa kanisa. Walipofika
kwake, akawaambia, Ninyi
wenyewe mnajua tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia, jinsi nilivyokuwa
kwenu wakati wote, nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi na
majaribu yaliyonipata kwa hila za Wayahudi; ya kuwa sikujiepusha katika
kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa, bali naliwafundisha waziwazi, na
nyumba kwa nyumba, nikiwashuhudia Wayahudi na Wayunani wamtubie Mungu, na
kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo.
Basi sasa, angalieni,
nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo
yatakayonikuta huko; isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema,
ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja. Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu
cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa
Bwana Yesu, kuishuhudia Habari njema ya neema ya Mungu. Na sasa, tazameni, mimi
najua ya kuwa ninyi nyote niliowahubiria ufalme wa Mungu, nikienda huko na
huko, hamtaniona uso tena. Kwa hiyo nawashuhudia wote siku hii ya leo, ya kuwa
mimi sina hatia kwa damu ya mtu awaye yote. Kwa maana sikujiepusha na
kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu.
Neno la Bwana...
Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 68 : 9-10, 19-20 (K)
32
K. Enyi falme wa dunia,
mwimbieni Mungu. Au: K. Aleluya.
Ee Mungu, ulinyesha mvua
ya neema;
Urithi wako ulipochoka
uliutia nguvu.
Kabila yako ilifanya kao
lake huko;
Ee Mungu, kwa wema wako
uliwaruzuku walioonewa. (K)
Na ahimidiwe Bwana,
Siku kwa siku
hutuchukulia mzigo wetu;
Mungu ndiye wokovu wetu.
Mungu kwetu sisi ni Mungu
wa kuokoa;
Na njia za kutoka
mautini. (K)
SHANGILIO
Yn. 14:16
Aleluya, aleluya,
Nitamwomba Baba, naye
atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele.
Aleluya.
INJILI
Yn. 17:1-11
Siku ile, Yesu aliinua
macho yake kuelekea mbinguni, akasema, Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze
Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe. Kama vile ulivyompa mamlaka juu ya
wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. Na uzima wa
milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo
uliyemtuma. Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa
niifanye.
Na sasa, Baba, unitukuze
mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu
kuwako. Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu;
walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika. Sasa wamejua ya kuwa
yote uliyonipa yatoka kwako. Kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa wao; nao
wakayapokea, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe
ndiwe uliyenituma. Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa,
kwa kuwa hao ni wako; na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; nami
nimetukuzwa ndani yao. Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo
ulimwenguni, nami naja kwako.
Neno la Bwana... Sifa
kwako Ee Kristu
-------------------------
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment