“KUFUFUKA NA KRISTO”
Tafakari ya Pasaka
Jumatano, Mei 19, 2021,
Juma la 7 la Pasaka
Mdo 20 : 28-38
Yn. 17:11-19
sala ya kuwaombea
wanafunzi
Ndugu wapendwa, karibuni
tena kwa tafakari ya neno la Bwana leo. Bado tupo katika kipindi cha Novena
tukimuomba Roho Mtakatifu na tunazidi kumshukuru kwa neema zake kwani kwa
hakika hata mimi (labda hata na wewe) umekwisha kuanza kuona matunda ya hizi
neema zipatikanazo kwa kusali novena kipindi hiki. Tuzidi kumwomba Mungu azidi
kutubariki.
Katika neno la Bwana leo,
tukianza na injili yetu, tunakutana na Yesu akiendelea kutoa sala ya kuwaombea
wanafunzi wake hali akijiandaa kuagana nao. Anaomba Mungu awalinde ili wabakie
katika umoja. Yesu mwenyewe anasema kwamba yeye alipokuwa pamoja nao aliwalinda
na kuwaongoza vyema. Alihakikisha kwamba hawadumbukii shimoni na alijitahidi
kweli lakini mmoja wao alikataa huu mwongozo wa Yesu na kuona kwamba hauhitaji
na hivyo akachagua njia yake mwenyewe na huko alikamatwa na shetani
aliyempotosha. Huyu ndiye Yuda Iscariot. Wale waliofuata mwongozo wake angalau
kidogo tu Yesu anaomba kwamba Mungu awalinde na yule mwovu na kuwatakasa katika
kweli.
Katika injili hii Yesu
anakuwa mfano kwetu kwamba kila aliyekabidhiwa na kundi, lazima ajiandae
kujitoa sadakaa kwa ajili yake na kuliongoza katika mwongozo sahihi. Sio
kuliacha ili liangamie. Hili linakuwa somo hasa kwa baadhi yetu ambao ni
viongozi; uongozi ni kujitoa sadaka, ni utayari wa kuhakikisha kwamba wenzangu
wanakula kwanza, wanapata mahitaji yao kwanza halafu mimi baadaye. Furaha yangu
ni pale wenzangu wanaposhiba kwanza na sio mimi nishibe. Kama mambo ndio yako
hivi, basi wengi wetu hapa kwa kweli tunahitaji tumwombe Mungu msamaha kwanza.
Hii ni kwa sababu wengi tunachukuliaga nafasi za cheo kama sehemu za sisi
kufaidi juu ya vichwa vya wengine. Hapa ni kutenda kinyume cha alivyotenda
Bwana wetu Yesu Kristo ambaye tunasema tunamwamini. Somo hili tena linatoa onyo
kali kwa wale akina baadhi yetu ambao tunatabia za kufanya mahusiano ya
kimapenzi hasa nje ya ndoa zetu. Unapofanya mapenzi na mtu, jua kwamba kuna
uwezekano wa kiumbe kuzaliwa. Wasichana wanaofanya mapenzi na wanaume wengi
wameishia kuzaa watoto ambao hata baba zao hawajulikani. Watoto wa namna hii
huishia kutekelekezwa. Najua ni kweli wengi wetu tunaudhaifu wa kutenda dhambi
hizi za kufanya mapenzi nje ya ndoa. Hii ni dhambi. Lakini dhambi inaongezeka
Zaidi pale ninapofanya mapenzi bila kutambua kwamba kile kitendo changu chaweza
kuzalisha tunda gani. Na je, huwa ninakuwa tayari kufuatilia kilichotokea baada
ya dhambi yangu ili niwe tayari kumtunza huyo mtoto. Jamani, kama umetenda
dhambi ya uzinzi/uasherati, basi fuatilia pia na yule mtoto atakayezaliwa ili
umtunze ili dhambi zisiongezeke zaidi kuliko kuacha yule mtoto azaliwe kama
asiyekuwa na Baba (kwa sababu labda mama atakuwa ametembea na wengi) na hivyo
yule mtoto kuteseka zaidi. Na kwa wale wazazi tunaowatelekezaga watoto tuache
tabia hizi. Tuige mfano wa Yesu.
Katika somo la kwanza
Paulo naye anatoa hotuba yake ya mwisho ambaye anajionyesha pia kama askari
mwaminifu aliyepigana kwa ajili ya Kristo huko Efeso. Hivyo anaondoka
akijisifia historia nzuri ya imani na mfano wa maisha. Hivyo anawaambia wale wa
Efeso kwamba ni kazi kwao. Kila linalohitajika alikwisha waonesha mfano. Hivyo
wanatakiwa watende kwa kadiri walichoona toka kwake na sio toka kwa waalimu wa
uongo ambao Paulo anasema kwamba wangeivamia Efeso. Hili ni somo kubwa kwetu.
Sisi tulipokeaga mfano mzuri toka kwa wazazi, waalimu wetu na wazee wetu.
Tujiulize, je hivi sasa ninatenda kuendana na kile alichonifundisha mama yangu?
Hivi kweli haya maisha ninayoishi sasa niliyajifunza au ninamuiga nani. Je,
ukataji wangu wa nywele unafanana na ule wa baba au mama yangu? Maneno yangu,
uvaaji wangu unafanana na ule wa mwalimu wangu? Hivi vimini ninaviiga kwa mama
yangu? Jiulize. Mara nyingi tunashindwa kwa sababu huwa hatuwaigi wale mifano
yetu ya kiimani. Tunaishia kuiga wanamuziki, wachezaji mpira, kila kitu tunaiga
kwao. Ukataji wa nywele wa wachezaji kama akina Balotel, jinsi wanavyochukuaga
wasichana mbalimbali, namna wanavyovaa, jinsi wanavyovaaga vimini, jinsi
wanavyofuga nywele, wanavyoongea, yote hayo. Hata akifukuza mke na wewe
unafukuza. Tambua tunu njema za imani kutoka kwa wazee wako walio kurithisha
imani. Tutafakari haya
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment