MASOMO YA MISA, MEI 19,
2021
JUMATANO YA 7 YA PASAKA
SOMO 1
Mdo 20 : 28-38
Paulo aliwaambia wakuu wa
kanisa ya Efeso: Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho
Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa
lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Najua mimi ya kuwa baada ya
kuondoka kwangu mbwamwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena
katika ninyi wenyewe watainuka watu, wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi
wawaandamie wao. Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na
mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi. Basi, sasa nawaweka katika
mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa
urithi pamoja nao wote waliotakaswa. Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi
ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji
yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa
kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya
Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.
Alipokwisha kunena haya akapiga magoti, akaomba pamoja nao wote. Wakalia sana
wote, wakamwangukia Paulo shingoni, wakambusu-busu, wakihuzunika zaidi kwa
sababu ya neno lile alilosema, ya kwamba hawatamwona uso tena. Wakamsindikiza
hata merikebuni.
Neno la Bwana...
Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 68:28-29, 32-35 (K)
32
(K) Enyi falme za dunia,
mwimbieni Mungu.
Au: Aleluya.
Ee Mungu, uziamuru nguvu
zako;
Ee Mungu, uwe hodari
uliyetufanyia makuu.
Kwa ajili ya hekalu lako
Yerusalemu
Wafalme watakuletea
hedaya. (K)
Enyi falme za dunia,
mwimbieni Mungu,
Msifuni Bwana kwa nyimbo.
Apandaye mbingu za mbingu
za tangu milele;
Aitoa sauti yake, sauti
ya nguvu.
Mhesabieni Mungu nguvu;
(K)
Enzi yake i juu ya
Israeli;
Na nguvu zake zi
mawinguni.
Mungu ni mwenye kutisha
Kutoka patakatifu pako.
Ndiye Mungu wa Israeli;
Yeye huwapa watu wake
nguvu na uwezo.
Na ahimidiwe Mungu. (K)
SHANGILIO
Yn. 14 : 26
Aleluya, aleluya,
Roho Mtakatifu
atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
Aleluya.
INJILI
Yn. 17:11-19
Siku ile, Yesu alisali
akisema: Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa; ili wawe na
umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina
lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule
mwana wa upotevu, ili andiko litimie.
Na sasa naja kwako; na
maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani
yao. Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa
ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.
Mimi siombi kwamba uwatoe
katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi
nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile
ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni. Na
kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli.
Neno la Bwana... Sifa
kwako Ee Kristo.
-------------------------
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment