MASOMO YA MISA, MEI 21,
2021
IJUMAA YA 7 YA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 25 :13-21
Siku zile, Agripa mfalme
na Bernike walifika Kiaisaria, wakimwamkia Festo. Na walipokuwa wakikaa huko
siku nyingi, Festo akamweleza mfalme habari za Paulo, akisema, Yupo hapa mtu
mmoja aliyeachwa na Feliki kifungoni; ambaye nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa
makuhani na wazee wa Wayahudi wakaniarifu habari zake, wakinitaka hukumu juu
yake. Nikawajibu kwamba si desturi ya Warumi kumtoa mtu awaye yote, kabla mtu
yule aliyeshitakiwa hajaonana na washitaki wake uso kwa uso, na kupewa nafasi
ya kujitetea katika mashitaka yake.
Basi walipokutanika hapa
sikukawia; bali siku ya pili nikaketi katika kiti cha hukumu nikaamuru mtu huyo
aletwe. Na wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lo lote baya, kama
nilivyodhani, bali walikuwa na maswali mengine mengine juu yake katika dini yao
wenyewe, na katika habari ya mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye
Paulo alikaza kusema kwamba yu hai. Nami nikaona shaka jinsi ya kutafuta hakika
ya habari hii, nikamwuliza kama anataka kwenda Yerusalemu ahukumiwe huko katika
mambo haya. Lakini Paulo alipodai kuwekwa ahukumiwe na Kaisari, nikaamuru
alindwe hata nitakapompeleka kwa Kaisari.
Neno la Bwana...
Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 103 :1-2, 11-12,
19-20 (K) 19
(K) Bwana ameweka kiti
chake cha enzi mbinguni. au: Aleluya.
Ee nafsi yangu, umhimidi
Bwana.
Naam, vyote vilivyo ndani
yangu
Vilihimidi jina lake
takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi
Bwana,
Wala usizisahau fadhili
zake zote. (K)
Maana mbingu zilivyoinuka
juu ya nchi,
Kadiri ileile rehema zake
ni kuu kwa wamchao.
Kama mashariki ilivyo
mbali na magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi
zetu mbali nasi. (K)
Bwana ameweka kiti chake
cha enzi mbinguni,
Na ufalmc wake
unavitawala vitu vyote.
Mhimidini Bwana, enyi
malaika zake,
Ninyi mlio hodari,
mtendao neno lake,
Mkiisikiliza sauti ya
neno lake. (K)
SHANGILIO
Kol. 3 :1
Aleluya, aleluya,
Mkiwa mmefufuliwa pamoja
na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa
Mungu.
Aleluya.
INJILI
Yn. 21 :15-19
Walipokwisha kula, Yesu
akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohane, wewe wanipenda kuliko hawa?
Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha
wanakondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili. Simoni na Yohane wanipenda?
Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo
zangu.
Akamwambia mara ya tatu,
Simoni wa Yohane, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya
tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa
nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.
Akasema, Amin, amin,
nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda
utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine
atakufunga na kukuchukua usikotaka. Akasema neno hilo kwa kuonyesha ni kwa
mauti gani atakayomtukuza Mungu. Naye akiisha kusema hayo, akamwambia, Nifuate.
Neno la Bwana... Sifa
kwako Ee Kristo.
-------------------------
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment