“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
Ijumaa, Mei 21, 2021,
Juma la 7 la Pasaka
Mdo 25: 13-21;
Zab 103: 1-2, 11-12,
19-20 (K. 19);
Yn 21: 15-19.
JE, WANIPENDA?
Karibuni ndugu zangu kwa
tafakari ya neno la Bwana katika siku ya leo tena. Bado tupo katika kipindi cha
novena tukimuomba Roho Mtakatifu na hadi sasa naamini tumekwisha anza kusikia
maisha yetu yakibarikiwa. Hivyo tuendelee kumwomba Roho Mtakatifu ili ifikapo
ile siku ya pentekoste, angalau na sisi tuweze kufurahia yaliyowatokea mitume.
Hili liwe ombi letu ndugu zangu. Na neno la Bwana leo katika somo la injili
tunamkuta Yesu akiongea na Simoni Petro katika hisia kali. Anamuuliza mara tatu
kama anampenda; anamueleza kwa hisia na msisitizo mkubwa sana. Anamuuliza je,
wanipenda-basi tunza kondoo wangu. Kama nilivyokwishadokeza katika tafakari
zilizopita, ni kwamba hapa Yesu alikuwa anataka kumpima Petro na kumweleza-je,
kweli umekuwa rafiki kwangu? Wewe kweli ni rafiki yangu? Kama ni rafiki yangu
ni lazima upende kile kilichomali yangu-yaani kondoo wangu. Hiki ndicho kipimo
cha urafiki.
Mara nyingi mtumwa
haonagi uchungu na kitu cha Bwana wake-yeye unaweza kumwambia akaoteshe mahindi
lakini yeye ataotesha mahindi kumi kumi kwenye shimo moja. Ukimwambia akubebee
labda mzigo wa gunia la mahindi akiona ni zito anaweza kulitoboa ili mahindi
yamwagike njiani ili uzito upate kumpunguka. Lakini rafiki asingefanya hivyo.
Rafiki atajitolea, kama ni mzigo mzito-ataona afadhali augawe mara mbili kuliko
kuutoboa na mahindi kumwagika barabarani. Ndivyo ilivyo kwetu sisi ndgu zangu.
Upendo wetu urafiki wetu na Yesu unaonekana kwa pale tuwapotayari kupenda kile
anachokipenda Yesu.
Ndugu zangu, sisi kwa
ubatizo wetu tuliahidi kuwa rafiki wa Yesu. Tuoneshe hili kwa kuwapenda kondoo
wake. Yesu anategemea tukikutana na kondoo wake akiwa na njaa, au kiu au katika
msongo wa mawazo tumfariji. Kumfariji kondoo hakuhitaji labda niwe na pesa ya
kumpa bali nitambue kwamba hata kauli yangu nzuri yaweza kumfariji kondoo kwa
namna ya ajabu. Tunatakiwa kuguswa kila tuonapo kondoo wa Yesu wakinyimwa uhai
kwa utolewaji wa mimba, wengine wakiwa wamekumbwa na utapiamlo, wengine
wakibebeshwa mimba katika umri mdogo, wengine wakijiingiza katika biashara ya
uasherati-tusifurahie kuwaangalia miili yao. Tuone huruma. Kufurahia kuangalia
miili ya kondoo hawa ni dalili ya roho ya muovu. Yote haya kama rafiki wa Yesu
ni lazima yatuguse.
Katika somo la kwanza,
tunakutana na Paulo akiendelea kushikiliwa kizuizini. Amefanya kazi yote ya
kuhubiri injili lakini udhia anaoupata ndio huu. Tutambue kwamba Paulo aliweza
kufikia hatua hii kwa sababu alielewa ukweli kwamba yeye ni rafiki wa Yesu.
Hivyo alikuwa tayari kila wakati kuitetea injili ya Bwana na kondoo wa Bwana.
Kwa tendo hili lake la kutoogopa vifungo au hata kifo au madhulumu, aliweza
kuwatia moyo wale wakristo wa mwanzo na kuwawezesha nao waihubri injili bila
kuogopa. Nasi tuepuke kuwa woga. Woga unawakwaza wale wanaokuja nyuma yako na
mwisho wa siku kazi ya injili inashindwa kusonga mbele. Sisi kama askari
walioko katika mstari wa mbele katika vita tuombe neema ya kuvumilia ili tuweze
kutoa mfano kwa wale walio nyuma yetu. Sisi tulio mbele endapo tutakimbia basi
kundi nzima nalo litarudi nyuma lote. Tuoneshe ujasiri na upendo wetu kwa
Kristo.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment