MASOMO YA MISA, MEI 20, 2021
ALHAMISI YA 7 YA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 22 : 30; 23 : 6-11
Wakati ule, Jemadari
alitaka kujua hakika, ni kwa sababu gani Paulo ameshitakiwa na Wayahudi,
akamfungua, akawaamuru wakuu wa makuhani na baraza yote wakutane. Akamleta
Paulo chini, akamweka mbele yao.
Paulo alipotambua ya kuwa
sehemu moja ni Masadukayo, na sehemu ya pili ni Mafarisayo, akapaza sauti yake
katika ile baraza, Ndugu zangu, mimi ni Farisayo, mwana wa Farisayo; mimi
ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu. Alipokwisha kunena hayo
palikuwa na mashindano baina ya Mafarisayo na Masadukayo, mkutano ukafarakana.
Kwa maana Masadukayo husema ya kwamba hakuna kiyama wala malaika wala roho;
bali Mafarisayo hukiri yote. Pakawa na makelele mengi. Waandishi wengine wa
upande wa Mafarisayo wakasimama, wakateta, w'akisema, Hatuoni uovu wo wote
katika mtu huyu; bali ikiwa roho au malaika amesema naye, ni nini? Ugomvi
mkubwa ulipotokea, yule jemadari akachelea Paulo asije akararuliwa nao,
akaamuru askari washuke na kumwondoa kwa nguvu mikononi mwao, na kumleta ndani
ya ngome.
Usiku ule Bwana akasimama
karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia
habari zangu Yerusalemu, imeku- pasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako.
Hilo ndilo neno la Mungu.
Neno la Bwana... Tumshukuru
Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 16:1-2, 7-11 (K) 1
(K) Mungu unihifadhi
mimi, kwa maana nakukimbilia Wewe. au: Aleluya.
Mungu unihifadhi mimi,
kwa maana nakukimbilia
Wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe
Bwana wangu,
sina wema ila utokao
kwako. (K)
Nitamhimidi Bwana
aliyenipa shauri,
Naam, mtima wangu
umenifundisha usiku.
Nimemweka Bwana mbele
yangu daima,
Kwa kuwa yako kuumeni
kwangu, sitaondoshwa. (K)
Kwa hiyo moyo wangu
unafurahi,
Nao utukufu wangu
unashangilia,
Naam, mwili wangu nao
utakaa kw;a kutumaini.
Maana hutakuachia kuzimu
nafsi yangu,
Wala hutamtoa mtakatifu
wako aone uharibifu. (K)
Utanijulisha njia ya
uzima;
Mbele za uso wako ziko
furaha tele;
Na katika mkono wako wa
kuume
Mna mema ya milele. (K)
SHANGILIO
Yn. 16:28
Aleluya, aleluya,
Nalitoka kwa Baba, nami
nimekuja hapa ulimwenguni; tena naucha ulimwengu, na kwenda kwa Baba.
Aleluya.
INJILI
Yn. 17 :20-26
Siku ile, Yesu alisali
akisema: Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu
ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami
ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba
wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na
umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe
wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma,
ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi.
Baba, hao ulionipa nataka
wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa;
kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu. Baba mwenye haki,
ulimwengu haukukujua; lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe
uliyenituma. Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo
lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.
Neno la Bwana... Sifa
kwako Ee Kristo.
-------------------------
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment