“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
Alhamisi, Mei 20, 2021.
Juma la 7 la Pasaka
Mdo 22: 30; 23: 6-11;
Zab 16: 1-2, 5-11 (K. 1);
Yn 17: 20-26
KWA NINI YESU ANASALI?
Ndugu zangu wapendwa,
karibuni katika tafakari yetu ya leo. Bado tunaendelea kufurahia kipindi cha
neema iletwayo na Roho wake Mungu kwa kipindi hiki cha Novena. Tuendelee
kumwomba Mungu kwa kipindi hiki. Na leo katika tafakari ya neno la Bwana
tukianza kwa kuiangalia injili yetu, leo tunamkuta Yesu akiendelea kuwaombea
wanafunzi wake. Na cha zaidi ni kwamba anawaombea na wale watakaofuata nyuma ya
wanafunzi wake. Anamuomba Mungu awashirikishe utukufu ule ambao atamshirikisha
yeye pia.
Hapa ndugu zangu twapata
maana ya kwa nini Yesu alituita rafiki. Yaani angalia anakuwa tayari kutuombea
sisi makao ya kuwa pamoja naye pale Baba alipomwahidia. Hii ni heshima kubwa
kwetu. Cha kumlipa ni sisi tupende utume wake. Yesu anataka injili yake na
upendo wake umfikie kila mmoja ulimwenguni. Kila kiumbe chake kionyeshwe
upendo. Kisiishi kwa kusumangwa bali kiufurahie ulimwengu; nacho kishirikishwwe
rasilimali za ulimwengu, kisaidiwe ili kiweze kukuza vipaji vyake na
kuvishirikisha ndani ya jamii, kikiugua kipendwe na kinaponyanyaswa atokee wa
kumtetea. Sisi kama rafiki wa Yesu tuwe mstari wa mbele katika kutekeleza hili.
Tumsaidie Yesu kama rafiki yetu ili lengo lake na nia yake hii iweze kufanikiwa
na kuwafikia wote.
Kingine ni kwamba ndugu
zangu kama Yesu anatuona rafiki kiasi cha kutushirikisha utukufu wake; yaani sisi
kuwako pale alipo-sisi nasi tuwe tayari basi kuwashirikisha wengine utukufu
wetu. Kuna baadhi yetu tuliojaliwa-lakini tunajifungia na kujitenga. Jaribu
kuwashirikisha wengine hizo raha zako na furaha zako. Ukiwa hotelini ukiwa
unakula nyama au divai yako na hapo kuna ombaomba anapita-usiache kumshirikisha
utukufu wako. Mnunulie na yeye angalau hata maji basi afurahie huo utukufu.
Ukiwa unapita njiani na gari yako halafu ukakutana na bibi kajitwika mzigo
mzito usiache kumshirikisha kautufu kako. Washirikishe watu utukufu wako na
Yesu atakushirikisha wa kwake.
Katika somo la kwanza
tunamkuta Paulo sasa amekamatwa, yuko kizuizini. Amefanya kazi kubwa ya
kuhubiri injili na watu wengi kawaokoa. Lakini sasa yuko kizuizini na bado Yesu
hajampatia pumziko. Lakini Paulo cha ajabu ni kwamba bado anamatumaini ya
ajabu. Anaona kama yote haya ni sehemu tu ya utume wake na hata hamlaumu Mungu
au kumwomba amwondoe huko kizuizini. Anajitetea kama mtu wa kawaida tu. Paulo
anayo mengi ya kutufunza. Kwenye utume au kwenye maisha ya kumfuata Kristo kuna
shida zake na hivyo tujifunze kuziona kama sehemu ya utume wetu. Wengi wetu
tunashindwa utume au kuishi kiaminifu maisha yetu kwa sababu hatujajifunza
kuzipokea shida kama sehemu ya utume. Maisha ya Paulo yawe kwetu changamoto za
kupambana na magumu ya kimaisha.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment