Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUNI 6, 2023


 
MASOMO YA MISA, JUNI 6, 2023
JUMANNE, JUMA LA  9 LA MWAKA
 

SOMO 1
Tob. 2:9 – 14
 
Tobiti alisema: Usiku ule ule nalirudi mazikoni, nikalala kwenye ukuta wa kiwanja changu, maana nimenajisika; na uso wangu hukufunikwa. Wala sikujua ya kama wamo videge katika ukuta, na macho yangu yalikuwa wazi. Hivyo videge wakatelemsha mavi ya moto ndani ya macho yangu; vikatokea vyamba vyeupe katika macho yangu. Nikaenda kwa matabibu wasiweze kunisaidia. Walakini Akiakaro alinilisha hata alipohamia Elimayo.

Basi mke wangu Ana alikuwa akifanya kazi ya kusokota vyumbani mwa wanawake, naye alipokwisha kazi huzipeleka kwao wenyewe. Wao wakamlipa mshahara; tena wakampa na zawadi ya mwanambuzi. Na yule mwanambuzi alipokuwamo nyumbani mwangu alianza kulia. Kwa hiyo nikamwuliza mke wangu, Huyu mwanambuzi ametokapi? Je! Hukumwiba? Uwarudishie wenyewe, maana si halali kula kilichoibiwa. Naye akanijibu, A-a, ni zawadi yangu niliyopewa faida zaidi ya mshahara wangu, Lakini mimi sikumsadiki; nikamwagiza awarudishie wenyewe; nikamwonea haya. Akarudisha maneno, Je! Wewe, zi wapi basi sadaka zako na matendo yako ya haki? Tazama ati! Umefahamika wewe na kazi zako zote.
 
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


 
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 112:1-2, 7-9 (K) 7
 
(K) Moyo wake u imara ukimtumaini Bwana.
Au: Aleluya.
 
Aleluya.
Heri mtu yule amchaye Bwana,
Apendezwaye sana na maagizo yake.
Wazao wake watakuwa hodari duniani;
Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa. (K)
 
Hataogopa habari mbaya;
Moyo wake u imara ukimtumaini Bwana.
Moyo wake umethibitika hataogopa.
Hata awaone watesi wake wameshindwa. (K)
 
Amekirimu, na kuwapa maskini,
Haki yake yakaa milele,
Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu. (K)


 
SHANGILIO
Zab. 147:12, 15
 
Aleluya, aleluya,
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu, huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya.


 
INJILI
Mk. 12:13-17
 
Walituma kwa Yesu baadhi ya Mafarisayo na Maherodi, ili wamnase kwa maneno. Hata walipofika walimwambia, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, wala hujali cheo cha mtu; kwa maana hutazami sura za watu; lakini katika kweli waifundisha njia ya Mungu. Je! Ni halali kumpa Kaisari kodi au siyo? Tumpe, tusimpe? Naye, akijua unafiki wao, akawaambia, Mbona mmenijaribu? Nileteeni dinari niione. Wakaileta. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Yesu akajibu, akawaambia, Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu. Wakamstaajabia sana.
 
Neno la Bwana... Sifa kwake Ee Kristu.
 
-------------------------
Copyright © 2023, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment