Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA JUNI 7, 2023


MASOMO YA MISA JUNI 7, 2023
JUMATANO, JUMA LA 9 LA MWAKA


SOMO 1
Tob. 3:1-10, 16-17

Tobiti alisikitika akalia, na katika huzuni yake aliomba akasema: Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye haki, na matendo yako yote na njia zako zote ni rehema na kweli, nawe unahukumu kwa kweli na kwa haki milele.

Unikumbuke, unitazame; usiniadhibu kwa ajili ya dhambi zangu na makosa yangu; wala kwa ajili ya dhambi za baba zangu walioasi mbele zako.

Kwa maana hawakuzitii amri zako; kwa hiyo umetutoa tuwe mateka, hata na kuuawa; kuwa mithali ya shutumu kwao mataifa yote, ambao kwamba tumetawanyika katikati yao.

Na sasa hukumu zako zi nyingi na za kweli; hata uje unitende kwa kadiri ya dhambi zangu na za baba zangu; kwa kuwa hatukuzishika amri zako; wala kuenenda kwa kweli mbele zako. Basi sasa unitende kama uonavyo vema; uniamuru niondolewe roho yangu, ili niruhusiwe na kuwa udongo tena; maana yanifaa kufa kuliko kuishi, kwa sababu nimesikia mashutumu yasiyo haki, nami naona huzuni nyingi.

Uamuru, basi, nitolewe katika msiba huu, niende mahali pa milele; wala usiugeuzie mbali nami uso wako.

Ikawa siku ile ile huko ekbatana, mji wa Media, Sara binti Ragueli naye alishutumiwa na wajakazi wa baba yake. Maana alikuwa ameolewa na waume saba, bali Asmodeo, yule jini, aliwaua kabla hawajalala naye. Wakamwambia, Wewe hujui ya kuwa umewanyonga waume zako? Umekuwa na waume saba, wala hata mmoja wao hukupata faida naye. Mbona waturudia sisi? Ikiwa wao wamekufa, nenda zako nawe ukawafuate; tusikuone kabisa una mwana wala binti. Alipoyasikia hayo alifanya huzuni nyingi, akaona afadhali kujinyonga. Akafikiri, Mimi ni binti pekee wa baba yangu; basi nikitenda hivi nitamwita shutumu; nitamshushia uzee wake kwa huzuni hata kaburini.

Basi ikawa sala zao wote wawili zilisikiwa mbele za enzi yake Mungu Aliye juu. Rafaeli akatumwa ili awaponye wote wawili.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. Zab. 25:2 – 9 (K) 1

(K) Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu.

Ee Mungu wangu,
Nimekutumaini Wewe, nisiaibike,
Adui zangu wasifurahi kwa kunishinda.
Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja;
Wataaibika watendao uhaini bila sababu. (K)

Ee Bwana, unijulishe njia zako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha.
Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu,
Nakungoja Wewe mchana kutwa. (K)

Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako,
Maana zimekuwako tokea zamani.
Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu,
Wala maasi yangu.
Unikumbuke kwa kadiri ya ujana wangu,
Wala maasi yangu.
Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako,
Ee Bwana, kwa ajili ya wema wako. (K)

Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake. (K)



SHANGILIO
Mt. 11:25

Aleluya, aleluya.
Nakushukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya.



INJILI
Mk. 12:18-27

Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, walimwendea Yesu, wakamwuliza na kusema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kwamba ndugu ya mtu akifa, akamwacha mkewe wala hana mtoto, ndugu yake amtwae yule mkewe akampatie ndugu yake mzao. Basi kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akatwaa mke, akafa, asiache mzao. Wa pili naye akamtwaa akafa, wala yeye hakuacha mzao. Na wa tatu kadhalika; hata na wote saba, wasiache mzao. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. Basi, katika kiyama atakuwa mke wa yupi katika hao? Maana wote saba walikuwa naye.

Yesu akajibu, akawaambia, Je! hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu? Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni. Na kwa habari ya wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma katika kitabu cha Musa, Sura ya Kijiti, jinsi Mungu alivyomwambia, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahi- mu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Hivyo mwapotea sana.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment