MASOMO YA MISA, APRILI 22, 2021
JUMA LA TATU LA PASAKA, ALHAMISI
SOMO 1
Mdo. 8:26-40
Malaika wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia, Ondoka
ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda
Gaza; nayo ni jangwa. Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi,
towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya
hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu, akawa akirejea,
ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya. Roho akamwambia Filipo,
Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo. Basi Filipo akaenda mbio,
akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma?
Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na
kuketi pamoja naye. Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili,
Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, na kama vile
mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, vivyo hivyo yeye naye
hafunui kinywa chake. Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani
atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi.
Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii
huyu asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu
mwingine? Filipo akafunua kinywa chake, naye, akakianza kwa andiko lilo hilo,
akamhubiri habari njema za Yesu.
Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji;
yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?
Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule
towashi; naye akambatiza. Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana
akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi.
Lakini Filipo akaonekana katika Azoto, na alipokuwa
akipita akahubiri Injili katika miji yote, hata akafika Kaisaria.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 66:8-9, 16-17, 20 (K) 1
(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.
Enyi mataifa, mtukuzeni Mungu wetu,
Itangazeni sauti ya sifa zake;
Aliyeiweka nafsi yetu katika uhai,
Wala hakuuacha mguu wetu usogezwe. (K)
Njoni sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu,
Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.
Nalimwita kwa kinywa changu,
Na sifa kuu zilikuwa chini ya ulinzi wangu. (K)
Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu;
Wala kuniondolea fadhili zake. (K)
SHANGILIO
Yn. 20: 29
Aleluya, aleluya,
Wewe Toma, umesadiki kwa kuwa umeniona, wa heri wale
wasioona, wakasadiki.
Aleluya.
INJILI
Yn. 6:44-51
Yesu aliwaambia Wayahudi: Hakuna mtu awezaye kuja
kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho. Imeandikwa
katika manabii, Na wote watakuwa wamefundishwa na Mungu. Basi kila aliyesikia
na kujifunza kwa Baba huja kwangu.
Si kwamba mtu amemwona Baba, ila yeye atokaye kwa
Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna
uzima wa milele.
Mimi ndimi chakula cha uzima. Baba zenu waliila mana
jangwani; wakafa. Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni; mtu akila chakula
hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya
uzima wa ulimwengu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2020, "MASOMO YA MISA" published
by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya
Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment