MASOMO YA MISA, APRILI 20, 2021
JUMA LA 3 LA PASAKA, JUMANNE
SOMO 1
Mdo. 7:51-8:1
Stefano aliwaambia Wakuu wa Makuhani: Enyi wenye
shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, sikuzote mnampinga Roho
Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo. Ni yupi katika
manabii ambaye baba zenu hawakumwudhi? Nao waliwaua wale waliotabiri habari za
kuja kwake yule Mwenye Haki; ambaye ninyi sasa mmekuwa wasaliti wake, mkamwua;
ninyi mlioipokea torati agizo la malaika msiishike.
Basi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo,
wakamsagia meno.
Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake,
akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono
wa kuume wa Mungu. Akasema, Tazama, naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu
amesimama mkono wa kuume wa Mungu. Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba
masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe.
Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli.
Wakampiga kw amawe Stefano, naye akiomba, akisema Bwana Yesu, pokea roho yangu.
Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha
kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 31:2-3, 5, 7, 16, 20 (K) 5
(K) Mikononi mwako naiweka roho yangu, ee Bwana.
Uwe kwangu mwamba wa nguvu,
Nyumba yenye maboma ya kunionkoa.
Ndiwe genge langu na ngome yangu;
Kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge. (K)
Mikononi mwako naiweka roho yangu;
Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.
Bali mimi namtumaini Bwana.
Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako. (K)
Umwangaze mtumishi wako,
Kwa nuru ya uso wako;
Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.
Utawaficha katika hema
Na mashindano ya ndimi. (K)
SHANGILIO
Yn. 10:14
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi mchungaji mwema, nao walio wangu nawajua,
nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.
INJILI
Yn. 6:30-35
Siku ile, Wayahudi walimwambia Yesu: Unafanya ishara
gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani? Baba zetu waliila mana
jangwani, kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale.
Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa
aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha
kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka
mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.
Basi wakamwambia, Bwana, sikuzote utupe chakula hiki.
Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa
kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2020, "MASOMO YA MISA" published
by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya
Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment