MASOMO YA MISA, APRIL 19, 2021
JUMA LA 3 LA PASAKA, JUMATATU
SOMO 1
Mdo. 6:8-15
Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya
maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi
lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale
wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza
kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye. Hata wakashawishi watu
waliosema, tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya kumtukana Musa na Mungu.
Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi;
wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza. Wakasimamisha mashahidi
wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa
patakatifu na juu ya torati; maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo
Mnazareti atapaharibu mahli hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa.
Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho
yao, wakamwona uso wake kuwa kama uso wa malaika.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 119: 23-24, 26-27, 29-30 (K)
(K) Heri walio kamili njia zao.
Wakuu nao waliketi wakaninena,
Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako.
Shuhuda zako ndizo furaha yangu,
Na washauri wangu. (K)
Nalizisimulia njia zangu ukanijibu,
Unifundisha amri zako.
Unifahamishe njia ya mausia yako,
Nami nitayatafakari maajabu yako. (K)
Uniondolee njia ya uongo,
Unineemesha kwa sheria yako.
Nimeichagua njia ya uaminifu,
Na kuziweka hukumu zako mbele yangu. (K)
SHANGILIO
Lk. 24:25-26
Aleluya, aleluya,
Ilimpasa Kristu kupata mateso haya, na kuingia katika
utukufu wake.
Aleluya.
INJILI
Yn. 6:22-29
Siku ya pili yake mkutano waliosimama ng’ambo ya
bahari waliona ya kuwa hakuna mashua nyingine huko ila moja; tena ya kuwa Yesu
hakuingia katika mashua ile pamoja na wanafunzi wake, bali wanafunzi wake
walikwenda peke yao. Walakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia mpaka
karibu na mahali pale walipokula mikate, wakati Bwana aliposhukuru. Basi
mkutano, walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia
mashuani wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu. Hata walipomwona
ng’ambo ya bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa?
Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni,
Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile
mikate mkashiba. Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula
kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo
ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu. Basi wakamwambia, Tufanyeje ili tupate
kuzitenda kazi za Mungu? Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu,
mmwamini yeye aliyetumwa na yeye.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
No comments:
Post a Comment