“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
Aprili 19, 2021.
------------------------------------------------
JUMATATU, JUMA LA 3 LA PASAKA,
Somo 1: Mdo 6:8-15 Shemasi Stefano, akitenda ishara
kubwa na miujiza kati ya watu, na kufanya watu walumbane katika Sinagogi.
Wimbo wa Katikati: Zab 119:23-24,26-27,29-30 Heri
ambao maisha yao hayana hatia.
Injili: Yn 6:22-29 Yesu anaendelea na katekesi yake
kuhusu Ekaristi.
------------------------------------------------
KUKUTANA NA MCHUNGAJI MWEMA ANAYETAKATISHA ROHO ZETU
Yesu
anatupatia fundisho ambalo kwa paska yetu tunaweza kulitumia kama dhihirisho
kwamba kweli tumefufuka na Kristo. Yesu baada ya kuwalisha watu wengi mikate na
baada ya wengi kutaka kumfanya mfalme, leo wanaendelea kumtafuta; wanamtafuta
wakifikiria kwamba atawapatia tena chakula. Hivyo hata lile lengo lao kutaka
kumfanya mfalme ni kwamba walitaka ili labda awe akiwatengenezea chakula kwa
miujuiza ili wao wale bila kufanya kazi. Yesu anatambua wanamtafuta kwa sababu
ya chakula na si kwa kiu ya neno la Mungu. Naye anawaambia wazi katika lugha
nzuri na ya kiupendo bila kufoka au kuchukia. Anawaambia watafute chakula cha
kiroho chenye kutolewa na Yesu.
Japokuwa
makutano walimtafuta Yesu kwa lengo la chakula cha kimwili, tukumbuke kwamba
uwepo wao karibu na Yesu uliwapa bahati ya kufundishwa na kupatiwa chakula
kifaacho. Kitendo cha kuwa karibu na maeneo matakatifu chaweza kubadili maisha
yetu; mazingira yanaweza kutoa nafasi ya Yesu kuongea nasi na kubadili nia zetu
na kuwa bora zaidi. Yapo maeneo au mazingira ambayo tukikaa karibu nayo-huwa
vigumu kwa Bwana kuzungumza nasi. Kuhudhuria kanisani, kushika vitu vitakatifu
kama rozari, au kuviweka chumbani mwetu au kwenye gari-vyaweza kutubadilisha.
Hivyo,
tupende kukaa katika maeneo matakatifu. Tutambue kwamba ukipoteza uhai wako
ukiwa ndani ya kanisa-wengi watakutangaza kama shahidi. Lakini ukipotezea uhai
wako ndani ya vilabu vya pombe–kwa wengi utaonekana kuwa mlevi. Tupendelee
kukaa katika maeneo Matakatifu ili tuweze kushindana na vishawishi vyetu.
Mazingira yaweza kutufanya pia tukaanguka kwenye dhambi kirahisi. Kama unataka
kutembea, pita barabara ambayo unajua itakuwa nzuri kwako itakusaidia ili uweze
kutembea vizuri, maisha ya kiroho yapo hivyo hivyo, tupite barabara ambayo
itatusaidia kushindana na vilema vyetu.
Tumsifu Yesu Kristo.
Copyright ©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki:
see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment