“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Kwaresima
Jumanne, Machi 9, 2021,
Juma la 3 la Kwaresima
Dan 3:25,34-43;
Zab 25:4-9;
Mt 18:21-35
MSAMAHA
Karibuni sana wapendwa
kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la
kwanza tunakutana na sala aliyoisali Azariah akiwa katika tanuru la moto baada
ya kutupwa huko na mfalme Nebuchadnezer kwa sababu ya kumtukuza Bwana Mungu wa
Israeli.
Azariah alimtumikia na
kumwamini Bwana Mungu na leo anashuhudia ulinzi wake maishani, anamfanya
asiaibike machoni pa adui zake. Kwa Azariah, huu ulikuwa wakati mgumu wa
kujaribiwa lakini alilia na Bwana na Bwana alimuokoa.
Sisi tujiombee ili tuwe
na imani kama ya Azariah kila tukumbanapo na vishawishi au adui maishani mwetu.
Vishawishi vinatukumba kila siku na kuishia kutushinda. Ni jambo la fedheha
kuanguka mikononi mwa adui zako. Wengi wetu tumekuwa tukiabika kwa kushindwa na
adui zetu. Tumwombe Mungu ili tusiaibike, tutoke kifua mbele.
Katika somo la injili,
Yesu anaelezea habari za mtumishi aliyesamehewa deni kubwa na baadaye kukataa
kusamehe mwenzake deni dogo. Huyu mtumishi wa kwanza aliyesamehewa deni kubwa
yaonekana alikuwa na deni kubwa ajabu. Hili deni inaonekana kwamba alilirithi
toka kwa ndugu au wazazi wake. Hivyo likamuangukia yeye kulipa. Ndio sababu za
hili deni kuwa kubwa hivi. Lakini alipoomba msamaha alisamehewa na hivyo alipaswa
kuonesha kwa mwenzake huruma kama iliyomtokea na kwake pia.
Yesu anatumia mfano huu
kuelezea hali yetu kama wanadamu kwamba tunapaswa kusamehe kwani sisi ndio
tuliosamehewa deni kubwa na Mungu. Sisi tulirithi deni la dhambi toka kwa
wazazi wetu wa mwanzo-Yesu ndiye aliyekufa msalabani kutufutia deni hili. Bei
ya deni hili lilikuwa kubwa sana kiasi kwamba sisi kama sisi hata kama
tungalifanya nini hakika hatungaliweza kulipa. Yesu ametulipia deni hili. Sisi
ndio tuliosamehewa deni kubwa na hivyo yatupasa kuwasamehe wenzetu.
Wapo wenzetu wenye mtindo
mbaya wa kudai, tunadai hadi senti ya mwisho. Tunatumia lugha mbaya katika
kudai, leo tunakumbushwa kwamba tutambue kwamba sisi nasi tumewahi kusamehewa
madeni tena makubwa kabisa. Hivyo tuwe na utayari wa kuwasamehe wenzetu. Yesu
anadhihirisha kwamba tunapokosa utayari wa kuwasamehe wenzetu-ni hasara kwetu
kwani tunajifufulia tena ile adhabu tuliyostahili kutokana na madhambi yetu.
Sisi tusiache kuwasamehe wenzetu.
Tunapojisikia hali ya
kutokusamehe-ni lazima kutambua kwamba ni shetani ametuingilia, na lengo lake ni
kutuvika kiburi ili aturudishe katika utumwa wa lile kosa la mwanzo. Shetani
anatafuta watumwa, sisi tusikubali tena kuwa watumwa wake kwakushindwa
kuwasamehe wenzetu.
Ukweli ni kwamba ulimwenguni
bila kusamehe hatutaweza kuendelea na maisha. Wanadamu ni dhaifu mno, hata yule
tunayemtegemea kwamba hawezi kutenda dhambi fulani atatenda. Baadhi ni wadhaifu
ajabu-unaweza kusema ni nini kipo vichwani mwao? Ni nini kimeingia huko .
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment