MASOMO YA MISA, MACHI 9,
2021
JUMANNE, JUMA LA 2 LA
KWARESIMA
SOMO 1
Dan. 3:25, 34-43
Ndipo Azaria akasimama
akasali hivi, akifumbua kinywa chake katikati ya moto na kusema:
Usituache kabisa, kwa
ajili ya jina lako, wala usilitangue agano lako na kutuondolea rehema zako, kwa
ajili ya Ibrahimu umpendaye, na kwa ajili ya Isaka mtumishi wako, na Israeli
mtakatifu wako kama nyota za mbinguni na kama mchanga wao pwani. Maana sisi, Ee
Bwana, tumekuwa duni kuliko mataifa yote, na kudhulumiwa leo katika ulimwengu
wote kwa sababu ya dhambi zetu. Sasa hakuna mfalme wala nabii wala kiongozi;
hakuna dhabihu wala kafara wala sadaka wala uvumba; wala mahali pa kukutolea
dhabihu na kuona rehema.
Lakini kwa moyo
uliovunjika na kwa roho nyenyekevu tukubaliwe nawe, na sadaka yetu iwe machoni
pako leo kama dhabihu za kondoo waume na ng’ombe, na kama kondoo wanono elfu
kumi. Nasi tukufuate kwa unyofu, maana wanaokutumaini Wewe hawataaibika.
Na sasa tunakufuata kwa
moyo wote; tunakucha na kuutafuta uso wako. Usitufedheheshe, bali ututendee kwa
kadiri ya fadhili zako, sawasawa na wingi wa huruma zako. Utuokoe kwa kadiri ya
maajabu yako, na kulitukuza jina lako, Ee Bwana.
Neno la Bwana… Tumshukuru
Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 25:4-9 (K) 6
(K) Ee Bwana, kumbuka
rehema zako na fadhili zako.
Ee Bwana unijulishe njia
yako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli
yako,
Na kunifundisha. (K)
Ee Bwana kumbuka rehema
zako na fadhili zako,
Maana zimekuwako tokea
zamani.
Usiyakumbuke makosa ya
ujana wangu,
Wala maasi yangu.
Ee Bwana, kwa ajili ya
wema wako. (K)
Bwana yu mwema, mwenye
adili,
Kwa hiyo atawafundisha
wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza
katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha
njia yake. (K)
SHANGILIO
Yn. 11:25, 26
Mimi ndimi ufufuo na
uzima, asema Bwana; Yeye aniaminiye mimi, hatakufa kabisa na milele.
INJILI
Mt. 18:21-35
Petro alimwendea Yesu
akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara
saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.
Kwa sababu hii ufalme wa
mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake.
Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye
alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake,
na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka,
akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa
mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni.
Mtumwa yule akatoka,
akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia; akamkamata, akamshika koo,
akisema, Nilipe uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi
akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda,
akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni.
Basi wajoli wake
walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao
yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu,
nimekusamehe wewe deni ile yoe, uliponisihi; nawe pia haikukupasa kumrehemu
mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika,
akampeleka kwa watesaji, hata atakapolipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu
wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehekwa mioyo yenu kila mtu ndugu
yake.
Neno la Bwana… Sifa kwako
Ee Kristo.
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment