“ASALI ITOKAYO MWMABANI”
Tafakari ya Kwaresima
March 8 2021.
JUMATATU, JUMA LA 3 LA
KWARESIMA
KUINGIA KATIKA MAPENDO NA
YESU!
Karibuni ndugu zangu kwa
adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana tutaanza kwa
kuliangalia somo la kwanza ambapo tunasikia juu ya kuponywa kwa mkoma aitwaye
Naamani. Mkoma huyu aliponywa tu baada ya kuwa mnyenyekevu, baada ya kusikiliza
kile Mungu anachosema, baada ya kusikiliza kile nabii anachosema. Hiki ndicho
kilichokuwa sababu ya Baraka kwake. Tunaona kwamba kutii kulimwia vigumu kwani
aliambiwa kitu ambacho machoni pa wengi kilionekana kama kinamshusha hadhi,
yeye mwenyewe na taifa lake, kwamba maji ya mito ya nchini mwake sio bora
kuliko ya Israeli. Yeye alipoambiwa akajichovywe kwenye hiyo mito alikasirika.
Lakini alipokubali mambo yalimwia vizuri. Hili ni fundisho kubwa kwetu ndugu
zangu kwamba endapo nasi tutakuwa tayari kuisikiliza sauti ya Bwana, basi hili
litakuwa chanzo cha Baraka kwetu. Mara nyingi tumemzuia Bwana kufanya kazi kwa
sababu tumeshampangia Bwana tayari utaratibu wa namna anavyopaswa kufanya kazi.
Hili limetuletea wengi madhara makubwa.
Katika Injili, Yesu
anasifu tukio la Naamani na anaongezea tena na tukio la Mama mjane wa Zerepta.
Wote wawili walikuwa tayari kuachana na mipango ya vichwa vyao na kumwacha
Mungu afanye kazi na nakwambia na kama wote wangekataa kumsikiliza Mungu na
kufuata mipango ya vichwa vyao, hakika wangeangamia-Naamani angeangamizwa kwa
ukoma wake na Mama mjane wa Zerepta angeangamizwa na njaa na kufa. Hili ni
fundisho kwetu. Pale tutakapofungua milango kwa ajili ya Bwana hakika Bwana
atafanya kitu na kuja kati yetu na kutubariki Zaidi na Zaidi. Tumsifu Yesu
kristo
Copyright ©2013-2020
©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment