“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumamosi, Februari 6, 2021,
Juma la 4 la Mwaka wa
Kanisa
KUMBUKUMBU
YA WAT. PAULO MIKI NA WENZAKE (MASHAHIDI)
Ebr 13: 15-17, 20-21;
Zab 22: 1-6;
Mk 6: 30-34.
YESU MWENYE HURUMA!
Karibuni
sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana katika adhimisho la Misa
Takatifu. Katika zaburi yetu leo ya wimbo wa katikati, mzaburi anatueleza
kwamba Bwana Mungu ni mchungaji wake. Na hakika hakuna awezaye kumshinda akiwa
mikononi mwa Bwana. Hii ni zaburi iliyoimbwa na Daudi katika imani kubwa.
Aliimba akiwa katika mapango akiwindwa auawe na mfalme Sauli. Daudi alimlilia
Mungu kwa zaburi hii na hakika Sauli alishindwa. Daudi alipatwa na maadui
wengi, alisalitiwa na wengi lakini hakuna aliyeweza kumshinda.
Leo
anatutolea ushuhuda kwamba kila amtumainiye Bwana, amfanyaye Bwana kuwa
mchungaji wake hakika atashinda tu. Zaburi hii inatumika leo kusisitiza ujumbe
wa somo la kwanza-toka waraka kwa waebrania kwamba wakristo wanapaswa
kujikabidhi kwa Yesu kwani yeye ndiye mchungaji mwema. Pia wawaheshimu viongozi
wao na kuwatii. Watambue kwamba Mungu amewapatia baadhi ya wanadamu wao
madaraka. Na hawa ni wachungaji kwa kundi lote. Hivyo wanapaswa kuwatii,
wasijiamulie wenyewe, wasiishi bila utaratibu.
Ndugu
zangu kwetu Kristo ni mchungaji mwema. Lakini shida ya sasa ni kondoo kukataa
maongozi ya mchungaji, kuishi wanavyotaka. Dunia inaharibika kwa sababu ya
kondoo kukataa maongozi ya wachungaji. Kristo ndiye mchungaji mkuu, lakini pia
kayakabidhi madaraka hayo kwa wanadamu wenzetu na jamii. Tuishi kuendana na
utaratibu, heshimu viongozi walioko ndani ya jamii. Kondoo lazima wasikie sauti
ya mchungaji. Wengi wetu tunafanya vitu ovyo kwa sababu hatufuati sauti ya
mchungaji.
Yesu
katika injili anadhihirisha kuwa mchungaji mwema, mwenye kukubali hata kutoa
muda wake wa kupumzika kwa ajili ya kondoo. Leo katika injili tunaona kwamba
alikuwa wamepanga kwenda mahali pa faragha na mapumziko lakini uwepo wa watu
unamsukuma kuwahudumia tu. Sisi tuache ubinafsi. Mara nyingi tukishapanga
ratiba zetu tunakuwa wakali watu kutuingilia. Lakini wakati mwingine ni
ubinafsi tu. Tuache ubinafsi, ratiba zetu zisitunyime tuache kuwafikia wenzetu.
Amina.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment