MASOMO YA MISA, FEBRUARI 6,
2021
JUMAMOSI, JUMA LA 4 LA
MWAKA
KUMBUKUMBU
YA WAT. PAULO MIKI NA WENZAKE (MASHAHIDI)
SOMO 1
Ebr. 13:15 – 17, 20 – 21
Kwa njia yake Yesu tumpe
Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake.
Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo
zimpendezazo Mungu.
Watiini wenye kuwaongoza,
na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu
watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua;
maana isingewafaa ninyi.
Basi, Mungu wa Amani
aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la
milele, yeye Bwana wetu Yesu, awafanye ninyi kuwa wakamilifu katika kila tendo
jema, mpate kuyafanya mapenzi yake; naye akifanya ndani yetu lipendezalo mbele
zake, kwa Yesu Kristo; utukufu una yeye milele na milele. Amina.
Neno la Bwana… Tumshukuru
Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 23 (K)
(K) Bwana ndiye mchungaji
wangu, sitapungukiwa na kitu.
Bwana ndiye mchungaji
wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani
mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu
huniongoza,
Hunihuisha nafsi yangu.
(K)
Aliniongoza katika njia
za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam, nijapopita katika
ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya,
Kwa maana Wewe upo pamoja
nami.
Gongo lako na fimbo yako
vyanifariji. (K)
Waandaa meza mbele yangu
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani
pangu,
Na kikombe changu
kinafurika. (K)
Hakika wema na fadhili
zitanifuata
Siku zote za maisha
yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa
Bwana milele. (K)
SHANGILIO
Zab. 119:105
Aleluya, aleluya,
Neno lako ni taa ya miguu
yangu, na mwanga wa njia yangu.
Aleluya.
INJILI
Mk. 6:30-34
Mitume walikusanyika
mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na mambo yote
waliyoyafundisha. Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha; mahali pasipokuwa
na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda,
hata haikuwako nafasi ya kula. Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa
na watu. Watu wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio
kwa miguu, toka miji yote, wakatangulia kufika. Naye aliposhuka mashuani,
akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na
mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi.
Neno la Bwana… Sifa kwako
Ee Kristu.
-------------------------
Copyright
© 2020, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora
– Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment