“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya kila siku
Jumatatu,
Februari 15 2021
Juma
la 6 la Mwaka wa Kanisa
Mwa
4: 1-15, 25;
Zab
50: 1, 8, 16-17;
Mk
8: 11-13
MIUJIZA
KUTOKA MBINGUNI!
Karibuni ndugu zangu
wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana
linaanza kwa kuiangalia Zaburi yetu ya Wimbo wa katikati toka zaburi ya 50.
Hapa tunakutana na Zaburi isemayo: umtolee Mungu dhabihu za kushukuru. Hii ni
amri, zaburi hii inasisitiza pia tena kwamba kila tujapo kwa Bwana kwa ajili ya
hii dhabihu, lazima moyo wetu uwe safi. Na hapa Bwana huipokea na kuibariki
dhabihu hii.
Leo katika masomo yetu,
anayetimiza hili ni Abeli. Yeye anakuja mbele ya Bwana na dhabihu ya kushukuru,
na anakwenda na moyo safi, na dhabihu yake inakubaliwa. Kaini anakwenda na moyo
mkaidi, na mara moja inakataliwa. Moyo wa uchoyo na hasira na chuki ndio
unaofanya dhabihu nyingi zisikubalike. Yawezekana Kaini alikwenda mbele za
Bwana na moyo kama huu. Bwana hakupokea dhabihu yake. Sisi tutambue kwamba ni
wajibu wetu kutoa dhabihu mbele ya Bwana. Sisi tuje mbele ya Bwana, tuondoe
chuki, na hasira na uchoyo. Uchoyo unaotukumba wengi ni kukataa kutoa mUda Wetu
kwa Bwana.
Kuna wakati kweli
tunanogewa na kazi, kazi inanoga tunamtupa Bwana pembeni. Pia tunakuja na chuki
sana na wengine-mbele ya Yesu hakuna haja ya kuhifadhi chuki kabisa. Huu ndio
udhaifu wetu, lakini inatupasa kuuleza mbele ya Bwana, tuukubali udhaifu huu.
Tumuombe atusaidie.
Kwenye somo la Injili,
Yesu anakataa kuwapatia ishara Wafarisayo. Yesu anakataa kuwapa ishara kwani
hii ilikuwa ni ishara kwa wasio na Imani, walitaka kumjaribu. Kati ya vitu
anavyovichukia Yesu ni kutaka kujaribiwa. Yeye anatenda muujiza kwa aliye na
imani. Hata siku moja hatendi muujiza kwa asiye na imani. Hiki kilichowapata
mafarisayo ndicho kinachotutokea na sisi kila siku ndugu zangu. Wengi wetu
hatujibiwi kwa sababu tunakwenda mbele ya Yesu bila imani.
Ukosefu wa unyofu
unatukosesha mengi, tukiwa mbele ya Yesu ni lazima tuoneshe unyofu. Yesu
alisema heri walio wanyofu wa moyo, maana watamuona Mungu. Unyofu wa moyo ni
kuishi kiapo chako bila kuonesha ufarisayo, bila kuwa ndumila kuwili, kama ni
watu wa ndoa tunaishi kama watu wa ndoa kweli. Sisi tukazane kuwa wanyofu.
Unyofu ni ufunguo wa baraka maishani mwetu.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment