MASOMO YA MISA, FEBRUARI
16, 2021
JUMANNE, JUMA LA 6 LA
MWAKA
SOMO 1
Mwa. 6:5 – 8, 7:1 – 5, 10
Bwana akaona ya kuwa
maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analoliwaza moyoni
mwake ni baya tu sikuzote. Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu
duniani, akahuzunika moyo. Bwana akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu
niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa
angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya. Lakini Nuhu akapata neema
machoni pa Bwana.
Bwana akamwambia Nuhu,
Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye
haki mbele zangu katika kizazi hiki. Katika wanyama wote walio safi ujitwalie
saba saba, mume na mke; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mume na
mke. Tena katika ndege wa angani saba saba, mume na mke; ili kuhifadhi hai
mbegu juu ya uso wa nchi yote. Kwa maana baada ya siku saba nitainyesha dunia
mvua, siku arobaini mchana na usiku; na kila kilicho hai nilichokifanya juu ya
uso wan chi nitakifutilia mbali. Nuhu akafanya kama vile Bwana alivyomwamuru.
Ikawa baada ya siku hizo
saba, maji ya gharika yakawa juu ya nchi.
Neno la Bwana… Tumshukuru
Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 29:1 – 4, 9 – 10,
(K) 11
(K) Bwana atawabariki
watu wake kwa Amani.
Sauti ya Bwana, enyi wana
wa Mungu,
Mpeni Bwana utukufu na
nguvu;
Mpeni Bwana utukufu wa
jina lake;
Mwabuduni Bwana kwa uzuri
wa utakatifu. (K)
Sauti ya Bwana I juu ya
maji,
Bwana yu juu ya maji
mengi
Sauti ya Bwana ina nguvu,
Sauti ya Bwana ina
adhama. (K)
Sauti ya Bwana
yawazalisha ayala,
Na ndani ya hekalu lake
wanasema wote, Utukufu.
Bwana aliketi juu ya
Gharika;
Naam, Bwana ameketi hali
ya mfalme milele. (K)
SHANGILIO
Zab. 25:4 – 5
Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, unijulishe njia
zako, unifundishe mapito yako.
Aleluya.
INJILI
Mk. 8:14 – 21
Wafuasi wake Yesu
walisahau kuchukua mikate, wala chomboni hawana ila mkate mmoja tu. Akawaagiza,
akasema, Angalieni, jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode.
Wakabishana wao kwa wao, kwa kuwa hawana mikate.
Naye Yesu akatambua,
akawaambia, Mbona mnabishana kwa sababu hamna mikate? Hamfahamu bado, wala
hamjaelewa? Je! Mioyo yenu ni mizito? Mna macho, hamwoni; mna masikio,
hamsikii? Wala hamkumbuki? Nilipoivunja ile mikate mitano na kuwapa wale elfu
tano, mlichukua vikapu vingapi vimejaa vipande? Wakamwambia, Kumi na viwili. Na
ile saba kuwapa wale elfu nne, mlichukua makanda mangapi yamejaa vipande?
Wakamwambia, Saba. Akawaambia, Hamjafahamu bado?
Neno la Bwana… Sifa kwako
Ee Kristo
-------------------------
Copyright
© 2020, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora
– Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment